WAPIGA KURA TUMIENI FURSA ZA UENDELEZAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

April 03, 2017  |   Latest News   |     |   0 Comment

Jaala Makame Haji ZEC .

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar inajukumu la kuandaa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria, Shughuli za uandikishaji wa wapiga kura wa Zanzibar na Uendelezaji Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zinaendeshwa kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba ya Zanzibar, 1984, sheria ya Uchaguzi, 1984 na Kanuni za Uendelezaji wa Daftari, 2008.

Uendelezaji wa Daftari ni shughuli ya kila siku inayofanywa na Tume baada ya shughuli ya uandikishaji wa wapiga kura kwa lengo la kuliweka sawa Daftari hilo ili liwetayari kutumika kwa ajili ya Shughuli za kiuchaguzi. Katika kuifanya shughuli hii ya Uendelezaji, Tume inaongozwa na Sheria ya Uchaguzi, 1984 na Kanuni ya Uendelezaji wa Daftari la Wapiga Kura, 2008.

Kanuni za Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura zinaeleza kwa Urefu juu ya Utaratibu mzima wa kuandikisha wapiga kura, utekelezaji wa shughuli nyengine za Uendelezaji wa Daftari la Wapiga Kura na kuweka fomu mbalimbali zinazotumika katika zoezi la uandikishaji na utaratibu wa kushughulikia maombi mbalimbali ya wapiga kura wanaoomba kupatiwa huduma katika uendelezaji huo wa daftari la Wapiga Kura.

Kazi za Uendelezaji wa Daftari la Wapiga Kura ilianzishwa baada ya kuwepo mfumo wa uandikishaji wa Wapiga Kura ambapo taarifa za Daftari hilo (taarifa za wapiga kura) ndizo zinazotakiwa kuendelezwa na kuwekwa sawa wakati wote kwa kuwaingiza wapiga kura wapya na kuwafuta waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari hilo, kushughulikia maombi ya Wapiga Kura hao na Maombi ya wapiga Kura waliopoteza Shahada zao za Kupigia kura.

Kimsingi shughuli hizi zinahitaji umakini mkubwa ili kuwa na ufanisi na kupatikana malengo yaliyokusudiwa, katika kuliona hilo Tume ilianzisha Afisi za Wilaya mwaka 2008 ambazo zina kazi ya kukusanya taarifa mbalimbali za wapiga kura waliofikia umri ili kuwaingiza katika Daftari kwa utaratibu maalum na kuwatoa katika Daftari wapiga Kura waliopoteza sifa kwa sababu ya kufariki au sababu nyengine kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, wahusika wakubwa wa kazi hii ya uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni pamoja na Afisi ya Mrajisi wa Vizazi na Vifo, Polisi, idara ya uhamiaji Afisi ya Sheha na Wapiga Kura wenyewe ambapo kila mmoja katika wahusika hao anaowajibu wake ambao utapelekea kazi ya uendelezaji wa Daftari hilo ikamilike kwa mafanikio yanayotakikana, jambo la msingi ni Ushirikiano na kila mmoja kutekeleza wajibu wake.

Tukumbushane kwamba, huduma zinazotolewa katika kazi za uendelezaji wa Daftari ni pamoja na kushughulikia uhamisho wa taarifa za mpiga kura ambae anahama kutoka eneo moja la Uchaguzi na Kuhamia eneo jengine la Uchaguzi ambapo taarifa za mpiga kura huyu zitawezwa kuhamishwa mara baada ya kufuata taratibu zilizowekwa na Tume ikiwemo kujaza fomu ambayo itakuwa na maelezo ya sheha wa shehia ambayo mpiga kura huyo amehamia yanayothibitisha tarehe,mwezi na mwaka wa kuhamia eneo hilo.

Huduma nyengine ya uendelezaji wa daftari ni kufanya masahihisho ya taarifa za Mpiga kura aliyeandikishwa katika daftari, Masahihisho hayo hutokana na kuandikwa visivyo kwa jina la Mpiga kura, anuani ya Mpiga Kura na taarifa nyengine ambazo zimeandikwa kimakosa. Katika fomu ya maombi ambayo itajazwa na mpiga kura ili kurekebishiwa taarifa zake atalazimika kuja anuani yake ya makaazi inayoonesha shehia, mtaa na nambari ya nyumba pale itakapolazimika kwa Afisa wa uandikishaji wa Wilaya kujiridhisha na Mpiga Kura huyo atawasiliana na sheha juu ya kupata taarifa sahihi za Mpiga Kura huyo.

Marekebisho mengine ya taarifa za mpiga kura hufanyika pale ambapo taarifa za mpiga kura zimebadilika kutokana na sababu za kimila,kidini,kiutamaduni (kwa mfano jina la ukoo kwa watu walioona,kubadilisha jina) au kubadilika kwa mipaka ya maeneo ya kiutawala. Mabadiliko ya jina na ukoo hakuhitaji msaada mkubwa kutoka kwa masheha.hata hivyo kunapotokea mabadiliko ya mipaka ya kiutawala ya shehia. Afisi za Wilaya zinahitajika kupata taarifa za kutosha za wapiga kura ambao watahamishiwa katika shehia mpya kutoka katika shehia za asili.

Aidha, daftari linahitaji kuendelezwa kwa kushughulikia maombi ya wapiga Kura waliopoteza shahada zao za kupigia kura, ili kuwa na ufanisi mkubwa wa huduma hii Afisi za Wilaya zinahitaji msaada mkubwa kutoka kwa masheha katika kushughulikia maombi ya Wapiga Kura waliopoteza shahada kwakuwa shahada hiyo ni miongoni mwa nyaraka muhimu za Serikali.

Zipo taratibu zilizowekwa na Tume kwa wapiga kura waliopoteza shahada zao ni kujaza fomu ambayo itahitaji kujazwa maelezo ya sheha na Polisi kwa madhumuni ya kuzuia udanganyifu wa baadhi ya wapiga kura. kwa upande wa Tume Mpiga Kura huyo atalazimika kulipa ada ya Tsh. 5,000/= ikiwa ni gharama za uchapishaji wa shahada mpya nyengine.

Afisi za Wilaya katika kazi za uendelezaji wa Daftari pia inajukumu la kupokea maombi ya kuwafuta wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Wapiga Kura pamoja na kupokea shahada zao, kazi hii haiwezi kufanikiwa bila ya kuwepo ushirikiano wa karibu na Sheha pamoja na jamaa wa karibu wa mpiga Kura aliyekosa sifa, jamaa huyo anaweza kuwa mtoto, ndugu,baba au mama. Mpiga kura anaweza kukosa sifa za kuwemo katika Daftari kwa sababu ya kifo au kuwa na uraia wananchi nyengine.

baada ya kukusanya taarifa za Wapiga kura waliopoteza sifa Tume huliweka wazi Daftari kwa kulibandika katika Afisi za Sheha na Afisi za Wilaya za Tume ili kila mwananchi aweze kuona, ajiridhishe na kutoa malalamiko yake kabla ya kufanyika zoezi la kuwafuta wapiga kura hao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Sheha anawajibu wa kuwaelimisha raia wake juu ya masuala haya ya uendelezaji wa daftari kwani kitendo hicho kitamrahisishia kazi Afisa Uandikisha wa Wilaya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mzuri zaidi.

Mpiga kura anawajibu wa kuhakikisha kwamba taarifa zake ziko sawa na zimenakiliwa kwa usahihi katika Daftari la kudumu la wapiga kura,kuelimisha wapiga kura wengine kuhusiana mwenendo mzima wa uendelezaji wa Daftari,kuihifadhi shahada yake ya kupigia kura ili isipotee na kuharibika kwa namna moja au nyengine.

Vile vile mpiga kura anawajibu wa kutoa msaada kwa wapiga kura wenye mahitaji maalum watakaohitajia kupatiwa huduma za uendelezaji wa Daftari katika Afisi za Tume za Wilaya sambamba na kutoa habari sahihi bila kujali jinsia,umri,ulemavu na tofauti nyengine yoyote ya kimaumbile.

Kwa upande wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia kitengo cha Elimu ya Wapiga Kura, habari na Uhusiano inafanya kila liwezokanalo kuhakikisha mpiga kura anapatiwa elimu sahihi inayohusiana na taratibu za uendelezaji wa daftari na kutoa taarifa sahihi zinazohitajika ili wapiga kura wengine washiriki kikamilifu katika kazi za Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

DSC04967

(Afisa Elimu ya Wapiga Kura  ZEC Ndg. Juma Sanifu Sheha akiwa katika semina ya masheha na wajumbe wao yenye lengo la kutoa elimu juu ya masuala ya Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.)

Kwa nia njema kabisa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawaomba wananchi na wapiga kura wote watumie fursa hii ya kuzijua haki na wajibu wao katika masuala ya uandikishaji na uendelezaji wa daftari la kudumu la Wapiga Kura.

Kwa wale wananchi ambao bado hawajaandikishwa katika daftari la Kudumu  na ambao tayari wametimiza sifa za kuandikishwa wajiandae kwa kutafuta kitambulisho cha uzanzibar mkaazi ili siku ikifika ya kuandikishwa wapiga kura wapya na wao wakajiandikishe hatimae wapate fursa ya kutumia haki ya kupiga kura wakati ukifika

Sambamba na hayo, kwa wale wanaohitaji kufanyiwa marekebisho ya taarifa zao au kuhamisha taarifa katika Daftari la Wapiga Kura wasikae na kusubiri tarehe za uandikishaji wakati hivi sasa fursa ipo ambayo ni uhakika kabisa kwani Afisa za uandikisha za Wilaya zipo wazi kwa ajili yao.

Inapaswa tujue kwamba, kazi za uendelezaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura inahusisha wadau mbalimbali wakiwemo masheha,wapiga kura,Asasi za kijamii,vyama vya siasa, vyombo vya habari na Taasisi za serikal hivyo, ni vizuri wadau hawa wakafanyakazi kwa ushirikiano wa karibu sana na Tume ya Uchaguzi ya Zanziba ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Related Posts

There is no related post.