WAZANZIBARI JIANDAENENI KUJIANDIKISHA KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA.

April 13, 2017  |   Latest News   |     |   0 Comment

Jaala Makame Haji ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada kwa kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa wadau wake wa Uchaguzi ili kila mwananchi aweze kuitumia haki yake kikamilifu katika shughuli za kiuchaguzi ikiwa ni pamoja na kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuidumisha amani iliyokuwepo ili iwe ni rahisi kwa serikali kuwaletea wananchi wake maendeleo yatakayo waridhisha.

Mwenyekiti Jecha aliyasema hayo tarehe 10 April 2017 katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Madungu wakati akifungua Semina ya siku moja ya Wanawake iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar juu ya masuala ya kiuchaguzi katika Nyanja za Uandikishaji wa Wapiga Kura na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

DSC05061

mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha akifungua Semina ya makundi ya wanawake kisiwani Pemba Tarehe 12.4.2017. (kulia ni Afisa Mdhamini ZEC Ndg. Ali Moh’d Dadi )

Naye Makamo mwenyekiti wa Tume hiyo Mh. Abdulhakim Ameir Issa, wakati akifungua semina ya siku moja ya  Vijana iliyotayarishwa na ZEC skuli ya Sekondar ya Madungu alisema jitihada za Tume ni kuitekeleza sera ya Ushirikishwaji  wa makundi maalum ili kila mwananchi apate elimu na taarifa sahihi kuhusu masuala ya kiuchaguzi

Akitoa maelezo mafupi katika semina ya vijana iliyofanyika tarehe 10 Aprili,2017 skuli ya Sekondari ya Madungu Afisa Sheria wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Ndugu Khamisi Issa khamis alisema hivi karibuni ZEC ilianzisha sera ya Ushirikishwaji wa Jinsia na makundi maalum lengo ni kutoa fursa kwa kila mwananchi aweze kutoa maoni yake kuhusu masuala ya kiuchaguzi.

Msaidizi Afisa Uandikishaji Wilaya ya Mjini Ndugu Muhammed Ali Abdallaha amewasihi wananchi kutoa taarifa sahihi za Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hasa zile taarifa za watu waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari la Wapiga Kura kwani kipindi hiki Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imo katika wakati wa kuwafuta wapiga kura waliopoteza Sifa.

Ndugu, Muhammed aliwaomba Wapiga Kura kujenga tabia kuzifuata Afisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya kwa madhumuni ya kutatua changamoto za kiuchaguzi ambazo zinawakabili na zinahitajia ufumbuzi wa haraka zaidi. Hata hivyo, Afisa Muhammedi alisema wapo vijana ambao hujaribu kuuza shahada zao za kupigia kwa wanasiasa jambo ambalo sio sahihi na linahatarisha mustakbali wa siasa ya Zanzibar.

Akiwasilisha mada katika semina ya Vijana iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Afisa Vijana Pemba Bibi Shuwena Hamadi Ali alisema, Vijana wanahaki ya kupewa elimu sahihi kuhusu masuala ya kiuchaguzi kwani vijana wengi wanaufahamu mdogo wa haki zao kwani hawako tayari kuitathmini na kuitumikia haki yao ya msingi ya kidemokrasia.

Bibi Shuwena alisisitiza kwa kusema elimu ya Uraia lazima iendelee kutolewa kwa Vijana ili vijana waache kurubiniwa na wanasiasa sambamba na kushauriwa na waandaliwe kisaicholojia kwa ajili ya kushiriki kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi yetu.

Aidha, Mjumbe wa Baraza la Vijana Micheweni ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano wa Baraza taifa Ndugu, Abdalla Khamis Shaame aliiomba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar isijeikashauriwa na viongozi wa kisiasa kuwatoa Masheha katika shughuli za kkiuchaguzi kwa kuangalia maslahi yao binafsi kwa Sheha anaumuhimu mkubwa hasa kwa masuala ya Uandikishaji wa Wapiga Kura.

DSC05109

Mjumbe wa mkutano mkuu Baraza la Vijana taifa Pemba Ndugu. Abdallah Khamis Shaame akichangia mada katika semina ya vijana madungu kisiwani Pemba. tarehe 12/4/2017.

Nao washiriki wa semina ya Wanawake ambayo pia iliandaliwa na ZEC waliwaomba wanawake wenzao kubadilika kwa kuwatayari kugombania nafasi za uongozi sambamba na kuacha kurubuniwa kwa kupewa hongo na wagombea wenzae wa kiume wakati wa Uchaguzi, kwani imekuwa kawaida wagombea wanawake wakiwa pamoja na wagombea wanaume wanakubali kupewa hongo na wanaume ili waache kugombea.

Semina za vijana na wanawake zimeandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango endelevu wa miaka mitano wa utoaji wa elimu ya Wapiga Kura.

 

 

Related Posts

There is no related post.