ZEC INAJIANDAA NA UCHAGUZI MKUU 2020.

April 13, 2017  |   Latest News   |     |   0 Comment

Jaala Makame Haji ZEC Zanzibar.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC ) Mh. Jecha Salim Jecha aliwahakikishia Wananchi wa Zanzibar kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa sasa inajitayarisha na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na hakutakuwa na Uchaguzi Mkuu mwengine kabla ya mwaka huo.

Mh. Jecha aliwasihi wananchi waache kudanganywa na viongozi wenye kutaka kuvunja amani iliyokuwepo katika nchi yetu na badala yake waendelee kufanya shughuli zao zitakazo waletea maslahi katika maisha yao na taifa kwa ujumla

Mwenye kiti Jecha aliitowa kauli hiyo wakati akifungua semina ya elimu ya Wapiga kura kwa makundi ya wanawake iliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha Elimu Mbadala Raha leo Mjini Unguja tarehe 13 Aprili, 2017. Semina hiyo ilitayarishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo, Ms. Afisa Uandikishaji Wilaya ya Mjini Ndugu, Mohammed Ali Abdalla aliwataka wapiga Kura kujenga tabia ya kuangalia Orodha za Wapiga Kura pale Tume inapoweka wazi orodha hizo ili wapate fursa ya kurekebisha taarifa zao na kuweka pingamizi dhidi ya orodha hizo pale patakapokuwa na haja ya kuweka pingamizi

Mkurugenzi wa Wanawake Bibi Nasima Chum aliwataka wanawake wenziwe kuacha kujiweka nyuma katika kupigania haki zao wasisubiri kupiganiwa na wanaume ikiwemo kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi yetu.  Katika Semina hiyo, Mkurugenzi Nasima aliwasilisha mada kuhusu nafasi ya wanawake katika kuleta maendeleo.

Mshiriki wa semina hiyo kutoka jumuiya ya SAVE NEW GENERATION Bibi. Siti Abbas Ali alisema wanawake wengi wanashindwa kugombea nafasi za uongozi kwa sababu ya ukosefu wa fedha na kutengwa katika vyama vyao hivyo alimuomba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Mh. Jecha Salim Jecha awasaidie wanawake kuingia katika nafasi mbalimbali za Uchaguzi sambamba na kuzidi kutoa elimu kwa Wanawake kuhusu mambo ya kidemokrasia.

DSC05292

mshiriki wa semina ya makundi ya wanawake Bibi. Siti Abbas Ali akichangia mada katika semina hiyo.

Akijibu masuala yaliyoulizwa na washiriki wa semina hiyo Afisa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Ndugu. Idrissa haji Jecha alisema tume haimbani mwanamke katika kushiriki masuala ya kiuchaguzi na ndiyo maana tume hiyo imeanziasha sera maalum kuhusu ushirikishwaji wa jinsia na makundi maalum.

Aidha, Afisa wa Wanawake kutoka Idara ya Wanawake Ndugu. Farashuu Juma Moh’d aliwashauri wanawake wenziwe kuanza harakati za kutafuta vitambulisho vya uzanzibari Ukaazi (ZAN ID) ili muda ukifika  wa Uandikishaji wa Wapiga Kura waweze kujiandikisha katika daftari hilo na wasisiburi kulalamika tu bila kuwafuatilia wenyewe.

Hata hivyo, aliwanasihi wanawake wenziwe waitumie Elimu waliyopewa na Tume ya Uchaguzi kuifikisha kwa wananwake wengine ili nao wafaidike na elimu hiyo nao kwa madhumuni ya kuitumia vyema haki ya kidemokrasia.

Semina za makundi maalum zinatolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa shughuli za utekelezaji wa Mpango endelevu wa utoaji wa Elimu ya Wapiga Kura mpaka mwaka 2020.

Related Posts

There is no related post.