KUUNDWA KWA TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliundwa kwa mujibu wa kifungu cha 119(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na kifungu cha 4 cha Sheria ya Uchaguzi Nam.11 ya 1984. Tume ya uchaguzi ya Zanzibar iliundwa tarehe 26 Machi, 1993 ikiwa na mwenyekiti ambaye ameteuliwa na Rais wa Zanzibar na Makamo mwenyekiti aliyechaguliwa na Wajumbe wa Tume kutoka miongoni mwa Wajumbe sita wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walioteuliwa na Mheshimiwa Rais.
Uteuzi wa Wajumbe wa Tume unadumu kwa kipindi cha miaka mitano tangu mjumbe alipoteuliwa ambapo Tume hii ni ya mwanzo kwa Zanzibar kuteuliwa kuendesha na kusimamia Uchaguzi kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambayo imeteuliwa tarehe 26 Machi,1993 na kumaliza kipindi chake cha cha miaka mitano ya utumishi tarehe 25 Machi,1998.
WAJUMBE WA MWANZO WA TUME.
Wajumbe wafuatao wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar waliteuliwa na Rais wa Zanzibar DK. SALMIN AMOUR JUMA tarehe 26 Machi,1993 :-
1. | Mwinyiwesa Idarous | Mwenyekiti |
2. | Ussi Khamis Haji | Makamo Mwenyekiti |
3. | Ahmada Khamis Hilika | Mjumbe |
4. | Hassan Haji Ali | Mjumbe |
5. | Issa Omar Suleiman | Mjumbe |
6. | Hassan Said Mzee | Mjumbe |
7. | Moza Himid Mbaye | Mjumbe |
Tarehe 21 Machi, 1995 Mhe. Mwinyiwesa Idarous na Mhe.Ussi Khamis Haji walijiuzulu kutokana na tuhuma za baadhi ya vyama vya siasa kwamba Tume imeelemea kwenye Chama tawala na hasa Mwenyekiti wake. Tuhuma hizi dhidi ya Tume zilipewa uzito na nguvu na baadhi ya wafadhili kutoka nje. Mhe.Rais wa Zanzibar alimteua Mhe. Zubeir Juma Mzee kuwa Mwenyekiti na Mhe. Ahmed Mohammed AbdulRahman kuwa mjumbe wa Tume kushika nafasi zilizoachwa wazi na Wajumbe waliojiuzulu.
Nafasi ya makamo mwenyekiti ilichukuliwa na Mhe. Hassan Said Mzee baada ya aliyekuwa makamo mwenyekiti kujiuzulu na kuteuliwa mjumbe mwengine wa Tume.