Na Jaala Makame Haji- ZEC

 Zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura limeanza rasmin katika Wilaya ya Magharib “A” pamoja na Jimbo la Kiwengwa, Mahonda na Bumbwini kwa Wilaya ya Kaskazini “B”

Wakizungumza katika vituo vya Uandikishaji baadhi ya Masheha wakiwa ni Mawakala wa Tume wamesema maandalizi mazuri ya Tume na kuimarishwa ulinzi na usalama katika vituo vyote kumesababisha wananchi kuhamasika na kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

Walisema pia, Utoaji wa Elimu na upatikanaji wa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na viongozi wa Shehia nako kumesaidia kutoa hamasa kwa wananchi kushiriki kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao.

Zoezi la Undikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa Wilaya ya Magharibi “A” pamoja na majimbo matatu ya Wilaya ya Kaskazini “B” litamalizika jumatatu ya tarehe 24/2/2020.

Wakati huo huo Wadau wa uchaguzi walishauri kuwa Matukio ya kiuchaguzi yanahitaji uvumilivu na ushirikiano baina ya Wadau wa Uchaguzi ikiwa pamoja na kutoa elimu ya wapiga kura ili kudhibiti na kutatua changamoto ambazo hujitokeza wakati wa Uchaguzi.

Ushauri huo ulitolewa na wadau hao katika Mkutano ulioandaliwa na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ukumbi wa kituo cha walimu Kiembe Samaki ukiwa na lengo la kutoa elimu kwa wadau wa Uchaguzi juu ya umuhimu wa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura.

Aidha, waliendelea kusema kuwa ushirikishwaji wa Wadau wa Uchaguzi katika hatua mbalimbali za uchaguzi utasaidia kupunguza changamoto na malalamiko ya wananchi ambayo hujitokeza kabla, wakati na baada ya Uchaguzi.

Akitoa ufafanuzi wa hoja zilizowasilishwa na wadau wa Uchaguzi katika mkutano huo Afisa Uandikishaji Wilaya ya Kusini MBARAKA SAID HASOUNI alisema, Tume itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo na kuhakikisha inazitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza wakati wa uchaguzi.

Afisa Uandikishaji Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MOHAMMEDI alisema huduma za uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambazo ni kuhamisha taarifa, kurekebisha taarifa na kushuhulikia maombi ya waliopoteza Vitambulisho vya Kupigia kura hazitofanyika katika katika vituo vya Uandikishaji badala yake huduma hizo zitafanyika katika Ofisi za Uchaguzi za Wilaya mara baada ya kumalizika kazi ya Uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura Vituoni.

Mkutano wadau wa Uchaguzi Wilaya ya Magharib "B" ni Mkutano wa kumi katika muendelezo ya mikutano ya wadau wa uchaguzi wa Wilaya iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya Uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa mpangilio wa Wilaya.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii