Na Jaala Makame Haji- ZEC
Masheha na mawakala kutoka Vyama vya siasa ambao watashiriki katika zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura Wilaya ya Kati wametakiwa kufuata miongozo na maelekezo waliyopatiwa na Tume ili kufanikisha zoezi hilo.
Afisa uandikishaji Wilaya ya Kusini MBARAKA SAID HASSOUN alitoa ushauri huo baada ya kuwaapisha mawakala hao katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Dunga Mkoa Kusini Unguja.
Alisema kazi ya uwakala inahitaji ushirikiano wa pamoja na makarani wa uandikishaji ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwa sambamba na kuwapatia wananchi haki yao ya kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Mawakala katika vituo vya uandikishaji vya Wilaya ya Kati wakila kiapo cha utendaji kazi mbele ya Afisa Viapo ambaye pia ni Afisa uandikishaji Wilaya ya Kusini MBARAKA SAID HASSOUN katika ukumbi wa Skuli ya Dunga Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 23/2/2020 (Picha na Jaala Makame Haji- ZEC)
Aidha, Afisa uandikishaji Wilaya ya Kati MUSSA ALI JUMA alisema Wapiga Kura wanaokwenda kuhakiki taarifa zao ni vyema kuwa na Vitambulisho vipya vya Mzanzibar Mkaazi na Kitambulisho cha Kupigia kura ambapo aliwata Wapiga Kura hao kuhakiki taarifa zao katika vituo walivyopigia kura kwa mara ya mwisho.
Mapema Mkuu wa kurugenzi ya tathmini na ufuatiliaji AMOUR AMEIR HAFIDHI aliwataka mawakala wa uandikishaji kuifanya kazi ya uandikishaji kwa mujibu wa taratibu na kuacha mitazamo na misimamo ya kisiasa ili kuwatambua watu wenye sifa za kuwemo katika Daftari la kudumu la Wapiga Kura.
Zoezi la unadikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura bado linaendelea kwa Wilaya Kaskazini “B” na Wilaya ya Magharibi “A” na lnatarajiwa kumalika kesho kwa Wilaya hizo.
Baada ya kukamilika katika Wilaya hiyo zoezi hilo litaanza katika Majimbo yote ya Wilaya ya Magharibi “B” na Jimbo la Tunguu kwa Wilaya ya Kati kuanzia tarehe 25/2/2020 mpaka tarehe 29/2/2020 ambapo majimbo mengine yaliyobakia kwa Wilaya ya Kati wataandikisha na kuhakiki taarifa zao pamoja na Majimbo ya Wilaya ya kusini Kuanzia tarehe 1/3/2020 mpaka tarehe 5/3/2020