Na Jaala Makame Haji - ZEC
Wananchi wa Majimbo yote ya Wilaya ya Magharib “B” pamoja na jimbo la Tunguu kwa Wilaya ya Kati wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya uandikishaji kwa ajili ya kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao
Wakatika akitembelea vituo vya uandikishaji Afisa uandikishaji wa Wilaya Magharib “B” KHAMIS MUSSA KHAMIS alisema matayarisho ya mapema na juhudi zinazochukuliwa na Tume katika kuwapatia wananchi taarifa mbali mbali za kiuchaguzi zimesababisha wananchi kujitokeza kwa idadi kubwa katika vituo vyote 38 vya Wilaya hiyo.
Mwananchi akiwa katika kituo cha kujiandikisha (Picha na Maktaba ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar)
Aidha, alisema mafanikio ya zoezi la uandikishaji yanatokana na ushirikiano uliopo baina ya afisi ya Tume ya Uchaguzi na Wakala wa usajili wa matukio ya kijamii kwa kuendelea kuwapatia wananchi vitambulisho vipya vya Mzanzibar Mkaazi katika kila Wilaya kufuatana na ratiba ya uandikishaji.
Baadhi ya Masheha wakiwa ni mawakala wa Tume ya Uchaguzi katika vituo vya uandikishaji waliwataka wananchi kuzitumia nambari zilizotolewa na Tume kwa ajili ya kuangalia vituo vyao vya kujiandikisha na kuhakiki taarifa kabla hawajafika katika vituo ili kuepuka usumbufu wa kutafuta vituo vyao kutokana na changamoto ya mgawanyo wa Shehia.
Sambamba na hayo, Masheha hao walitoa wito kwa wananchi kufuata malekezo yanayotolewa na Tume kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao kabla siku kumalizika
Nao wananchi wa Wilaya ya Magharib “B” waliofika vituoni kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao walisifu juhudi zinazochukuliwa na Tume kwa uamuzi wa kutumia mfumo mzuri wa uandikishaji ambao unasaidia zoezi hilo lifanyike kwa haraka zaidi.
Zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura waliokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura limeanza leo tarehe 25/2/2020 katika majimbo yote ya Wilaya ya Magharibi “B” pamoja na jimbo la Tunguu kwa Wilaya ya Kati ambapo linatarajiwa kudumu la siku tano mpaka tarehe 29/2/2020.