Na Jaala Makame Haji - ZEC

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Ali Mohamed Shein leo alikuwa ni miongoni mwa Wapiga Kura waliofika kituoni kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Dk.  Shein akifuatana na Mke wake Mama Mwanamwema Shein alifika kituo cha Skuli ya Bungi na kufuata taratibu zote za kuandikishwa ikiwemo kupanga foleni kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao zilizomo katika Daftari ambapo kituo hicho ndio kituo chao cha kawaida cha kupigia kura.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. ALI MOHAMED SHEIN (kulia) akiwa katika foleni kusubiri kuingia kituoni kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake  

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuhakikiwa Dk. Shein alikiri kuwa zoezi la Uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kuwa linaenda Vizuri kutokana na utaratibu mzuri na mfumo wa uandikishaji ulioandaliwa na Tume ya uchaguzi ambao unawapatia huduma wananchi kwa haraka zaidi.

Aidha, Dk. Shein alisema kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ni haki ya kila Mtu hivyo aliwatoa hofu wananchi ambao hawajapata vitambulisho vipya vya Mzanzibar Mkaazi na kuwaomba kuendelea kufatilia kutokana na umuhimu wake kwa matumizi mbali mbali.

Sambamba na hayo, Rais Shein alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiandaa kuendesha Uchaguzi ulio   huru na haki kutokana na kuandaliwa misingi bora ambayo itawawezesha wananchi kupata haki yao ya kupiga kura na kuwa na ridhaa ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa maslahi yao na taifa kwa jumla.

Akizungumzia suala la Amani na utulivu uliopo nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu alisema Serikali ya Mapinduzi haitokuwa tayari kuona baadhi ya Watu wanajaribu kuvuruga amani iliyopo na itaendelea kuwadhibiti na kuwachukulia hatua wale watakaofanya hivyo.

Katika hatua Nyengine Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe Jaji Mkuu Mstaafu HAMID MAHMOUD HAMID alipata fursa ya kutembelea vituo vilivyopo katika kisiwa cha Uzi ikiwa ni miongoni mwa hatua moja wapo ya Tume hiyo kuendelea na taratibu za kufuatilia zoezi hilo na kujionea baadhi ya changamoto zinazojitokeza

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Hamid alisema lengo la Tume ya Uchaguzi ni kuandikisha idadi kubwa ya Wananchi wenye sifa hivyo, itahakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto hizo.

Zoezi la Uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa Wilaya ya Magharibi “ B’ na jimbo la Tunguu kwa Wilaya ya Kati limemalizika leo ambapo zoezi hilo litaendelea katika Majimbo yaliyobakia ya Wilaya ya Kati na Majimbo yote ya Wilaya ya Kusini kuanzia tarehe 1/3/2020 mpaka 5/3/2020.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii