Na Jaala Makame Haji – ZEC.

Mkuu wa kitengo cha Huduma za Sheria Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ISSA KHAMIS ISSA alieleza kuwa Tume imeanzisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa lengo la Kukuza misingi ya Uchaguzi wa Kidemokrasia nchini.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Masheha na Mawakala wa vyama vya siasa watakaosimamia kazi ya Uandikishaji kwa Wilaya Mjini ambayo inatarajiwa kuanza tarehe 6/3/2020 alisema Daftari la kudumu la Wapiga Kura linasaidia kumjua mwananchi mwenye sifa za kuandikishwa na kuwemo katika daftari hilo ili kuweza kumchagua kiongozi anayemtaka siku ya Uchaguzi

 Alisema hivi sasa Tume inafanya uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura ikiwa na lengo la kuwatambua wapiga kura ambao hawana sifa za kuwemo katika Daftari na hatimaye kuwafuta katika Daftari hilo.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo juu ya maelekezo kwa Masheha na Mawakala Msaidizi Afisa Uandikishaji Wilaya ya Magharib “A” MWANAMKUU GHARIB MGENI alifahamisha kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Nam. 4 ya mwaka 2018, Sheha ana wajibu wa Kushirikiana na Mkuu wa Kituo na Makarani wa uandikishaji katika kuhakikisha kuwa Sheria na Kanuni zinazohusiana na mwenendo wa uandikishaji wa Wapiga Kura katika kituo cha Uandikishaji zinafuatwa.

 

Afisa uandikishaji Wilaya ya Mjini  SAFIA IDDI MUHAMMAD akizungumza katika moja ya mikutano ya  Wadau wa uchaguzi (picha na Maktaba - ZEC) 

Aidha, Bi Mwanamkuu aliongeza kusema kuwa, Masheha wakiwa ni Mawakala wa Tume na ni viongozi wa Serikali katika Shehia wanawajibu wa kuzielewa Sheria na taratibu za Tume zinazoendesha uandikishaji.

Naye Msaidizi Afisa Uandikishaji Wilaya ya Kati SAID RAMADHAN MGENI aliwaasa Mawakala kuachana na misimamo ya Kisiasa wanapokuwa katika vituo vya uandikishaji na badala yake kuifanya kazi hiyo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa

Afisa uandikishaji Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MUHAMMAD alisema, lengo la kutoa mafunzo kwa Mawakala ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume ya Uchaguzi

Zoezi  la uandikishaji kwa majimbo yote ya .Wilaya ya Kusini na majimbo mawili ya Wilaya ya Kati limeanza  leo na linatarajiwa kumalizika tarehe 5/3/2020.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii