Na Jaala Makame Haji - ZEC

Raisi Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.  ALI HASSAN MWINYI ameshiriki katika zoezi la uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura katika kituo cha Skuli ya Miembeni Shehia ya Muembe Madema.

Mhe. MWINYI akifuatana na Wake zake Mama SITI ABDALLA pamoja na Mama KHADIJA AMOUR KHALFAN baada ya kufanya uhakiki wa taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura aliwata Wananchi kuacha tabia ya kudharau na kupinga masuala ambayo yanamanufaa kwao na Taifa kwa jumla.

Alisema wakati tukielekea katika kipindi cha uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 wananchi wanawajibu wa kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao ili kuwa na uhakiki wa kupiga Kura katika hali ya Amani na utulivu.

Raisi Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali Hassan Mwinyi akipatiwa maelekezo na Mkuu wa kituo cha uandikishaji (kushoto) cha Skuli ya Miembeni Shehia ya Muembe Madema Wilaya ya Mjini - Zanzibar wakati alipofika kituoni hapo kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 11/3/2020 (Kuliani ni Wake wa Rais Mwinyi. Mama SITI ABDALLA na Mama Khadija Amour nao)

Naye Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. ZUBEIR ALI MAULID alifanya uhakiki wa taarifa zake katika Kituo cha Skuli ya Maandalizi Saateni Shehia ya Saateni Jimbo la Shauri Moyo ambacho ndicho kituo chake cha kawaida cha Kupigia Kura.

Baada ya kufanya uhakiki wa taarifa zake Mhe. Maulid alisema kujiandikisha ni jambo muhimu na ni haki wa Kikatiba ambayo inatoa fursa kwa mwananchi kuchagua kiongozi anayemtaka wakati wa Uchaguzi

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. ZUBEIR ALI MAULID akiwa katika kituo cha uandikishaji cha Skuli ya Maandalizi Saateni kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 11/3/2020 (Picha na Jaala Makame- ZEC)

Mheshimiwa Maulidi alifafanua kuwa Tume ya Uchaguzi inafanyakazi kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya uhuru na uwazi hivyo, aliwaomba wanasiasa na Wananchi kwa jumla kuendelea kuiamini Tume na endepo watakuwa na malalamiko wanapaswa kutumia vyombo husika badala ya kutumia mitandao kwa kuipotosha jamii.

Afisa uandikishaji Wilaya ya Mjini SAFIA IDDI MUHAMMADI alieleza kuwa, mafanikio ya kazi ya uandikidshaji katika vituo vyote 56 vya uandikishaji vya Wilaya hiyo yanatokana na ushirikiano uliokuwepo baina ya Tume ya Uchaguzi na Masheha katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo la uandikishaji

Zoezi la uandikishaji kwa Wilaya ya Mjini linakamilisha mzunguuko wa ratiba ya uandikishaji kwa Wilaya zote kumi na moja Unguja na Pemba ambapo Zoezi hilo kwa Wilaya ya Mjini limeanza leo tarehe 11/3/2020 na linatarajiwa kukamilika Jumapili ya tarehe 15/3/2020

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii