Na Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC imezitaka Taasisi zilizozoshiriki kuangalia Uchaguzi Mkuu kuwasilisha ripoti zao za uangalizi kwa kutoa mapendekezo yenye nia ya kujenga Amani na utulivu na kutanguliza  maslahi ya wananchi kuliko kueleza zaidi hisia za kisiasa.

Ushauri huo ulitolewa na Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Mabruki Jabu Makame katika Ukumbi wa Mikutano wa Tume hiyo Maisara Zanzibar mara baada ya kupokea ripoti ya waangalizi wa Uchaguzi Mkuu 2020 kutoka Jumuiya ya kupambana na Changamoto za Vijana Zanzibar ZAFAYCO.

Makamo Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa Changamoto na Mapendekezo yaliyowasilishwa katika ripoti za uangalizi zina lengo la kumarisha uendeshaji na Usimamizi wa Chaguzi zijazo

Hata hivyo, ZEC imezipongeza Taasisi za ndani ya nchi zilizoshiriki kuangalia Uchaguzi Mkuu 2020 kwa kuwa wa Mwanzo kutoa matamko juu ya mwenendo wa Uchaguzi kuliko taasisi za nje ya nchi hali ambayo ni tofauti na chaguzi zilizopita.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya ZAFAYCO Abdalla Ali Abeid alieleza kuridhishwa kwake na utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika kuendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu 2020 kwa vile Tume hiyo iliyashirikisha kwa karibu zaidi makundi ya Vijana kushiriki katika harakati za Uchaguzi.

Ndugu Abdallah alieleza kuwa, ZAFAYCO iliridhishwa na uamuzi wa ZEC wa kuondosha ukomo wa idadi ya Waangalizi kwa taasisi za Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu 2020 hali ambayo iliufanya Uchaguzi Mkuu 2020 kuwa huru na wazi katika hatua zote kuanzia Uandikishaji hadi upigaji kura.

Taasisi ya kupambana na changamoto za Vijana Zanzibar ZAFAYCO imewasilisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ripoti ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu 2020 uliofanywa na Waangalizi kutoka Taasisi hiyo.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii