Na. Jaala Makame Haji - ZEC

TUME YA UCHAGUZI ZANZIBAR, inawaomba wananchi , wapiga kura  wa jimbo la Pandani  , vyama vya Siasa , wagombea , na wadau wengine wa uchaguzi kujitayarisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi  mdogo wa jimbo hilo uliopangwa kufanyika tarehe 28 March 2021.

Akizungumza na Wadau wa Uchaguzi katika Ukumbi wa Jamhuri Wete Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Mkuu mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alisema, Uchaguzi huo unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Mwakilishi Mteule wa Jimbo hilo Mhe. Abuubakari Khamis Bakar kilichotokea 11 Novemba 2020.

 

Mhe. Mahmoud Alieleza kuwa   uchaguzi huo hautakuwa na  upigaji kura wa mapema kutokana na maelekezo ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018.

Naye Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo Mheshimiwa Mabruk Jabu Makame aliwaomba Wapiga Kura wa Jimbo la Pandani kuendelea kudumisha Amani mpaka kumalizika kwa Uchaguzi huo.

Akiwasilisha mada katika Mkutano huo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha huduma za Sheria Tume ya Uchaguzi Mbaraka Said Hassouni alifahamisha kuwa, ZEC baada ya kupata taarifa kutoka kwa Spika wa Baraza la Wawakilishi juu ya  kuwepo nafasi wazi ya mjumbe wa Baraza la Wawakilishi inawajibika kuendesha Uchaguzi huo kutokana na maelekezo  ya kifungu cha 40(2) na (3) cha Sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.

Nao wadau wa Uchaguzi wa Jimbo, wameishukuru Tume ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha vyema katika uchaguzi uliopita na kuiomba Tume hiyo kuendelea kuwasirikisha katika chaguzi zinazo fuata.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imetangaza kuwa tarehe 12 Machi, 2021 kuwa ni siku ya Uteuzi wa Wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni ambapo Kampeni za uchaguzi zitafanyika tarehe 13 Machi hadi 26 Machi, 2021.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii