Na. Jaala Makame Haji-ZEC

Waangalizi wa Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 wameshauriwa kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa pamoja na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa wakati wa kuwasilisha taarifa za uangalizi wa Uchaguzi.

Ushauri huo ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Saadun Ahmed Khamis wakati akipokea taarifa ya waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar JUWAUZA katika ukumbi wa Tume hiyo Maisara Mjini Zanzibar.

 

Bwana Saadun alisema, waangalizi baada ya kukutana na Tume, wanapaswa kukutana na Wadau wengine wa Uchaguzi wakiwemo vyama vya Siasa na Ofisi ya Msajili wa vyama ili kuwasilisha mapendekezo na changamo ambazo zinawahusu moja kwa moja wadau hao.

Aidha, Bwana Saadun alizidi kusema kuwa, Tume kwa upande wake imeyapokea na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kadri itakavyowezekana changamoto na mapendekezo yote yaliyowasilishwa na waangalizi wa Uchaguzi ili kuona uchaguzi unaofuata unakuwa huru na wa kuaminika.

 Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wenye ulemavu Zanzibar Bi Salma Saadat Haji aliishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiingiza elimu ya Wapiga Kura katika mtaala wa Elimu wa Skuli za Sekondari ili kuwafanya wanafunzi kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya Kidemokrasia katika nyanja ya Uchaguzi

Wakati akiwasilisha taarifa fupi ya matukio yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu 2020 Mtaalamu wa Mawasiliano katoka JUWAUZA Bi Hawra Mohammed Shamte aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kusimamia vyema uchaguzi Mkuu 2020 na kuwashirikisha kikamilifu watu wenye mahitaji maalumu katika uchaguzi huo.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imepokea taarifa ya Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu 2020 kutoka kwa Jumuiya ya Wanawake wenye ulemavu Zanzibar

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii