Na Jaala Makame Haji - ZEC

Viongozi na watendaji katika Taasisi za Umma wameshauriwa kuwa wazalendo na kufuata maadili ya Kiutumishi wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Ushauri huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Khamis Kona Khamis wakati akizungumza na Watendaji wa Tume hiyo katika ziara ya kuzitembela Afisi za Uchaguzi za Wilaya.

Mkurugenzi Khamis alisisitiza kuwa Uzalendo ndio nyezo muhimu kwa watumishi wa Umma kwani utapelekea maendeleo ya haraka kwa Taifa pamoja na kujenga Imani kwa Viongozi na Watumishi.

Ndugu Khamis aliongeza kusema, katika kuimarisha ushirikishwaji na ulinzi wa maeneo ya kazi ni vyema watendaji wa Taasisi za Serikali wakajenga uhusiano wa Karibu na Wadau wao pamoja na Watu wanaoyazunguuka maeneo yao  kwa ajili ya kurahisisha kazi zao.

Hata hivyo, Mkurugenzi Khamis Kona aliwaasa Watumishi hao kudumishi usiri wa kazi zao za kila siku ili kuepukana na matatizo yasiyokuwa ya lazima katika Afisi zao na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na hayo Mkurugenzi Khamis aliaahid kuzifanyia kazi changamoto zinazozikabili Afisi za Uchaguzi za Wilaya ili kusudi kuendana na hadhi ya Afisi hizo Kwa mujibu wa Sheria ya kuanzishwa Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Namb. 1 ya mwaka 2017.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Kurugenzi ya Rasilimali Watu, Mipango na Uendeshaji Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Saadun Ahmed Khamis aliwataka Watendaji wa Tume hiyo kufanyakazi kwa kushirikiana katika kuzitatua changamoto za Afisi hiyo.

Nao, Maafisa wa Uchaguzi wa Wilaya kwa nyakati tofauti walimpongeza Mkurugenzi wa Uchaguzi kwa kuamua kufanya ziara katika Ofisi zao na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa katika ziara hiyo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Khamis Kona alifanya ziara katika Ofisi za Uchaguzi za Wilaya ya Kusini, Kati na ghala dogo la Tume Kitogani kwa Mkoa Kusini Unguja, pamoja na Ofisi ya Uchaguzi ya Wilaya ya Magharibi “A” kwa Mkoa wa Mjini Magharibi.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii