Na Jaala Makame Haji – ZEC

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Ndg. Khamis Kona Khamis amewataka watendaji wa Tume hiyo kujenga tabia ya kuzisoma mara kwa mara Sheria, Kanuni, Sera na Miongozo za Uchaguzi kwa lengo la kuimarisha uweledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mkurugenzi aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo watendaji wa Tume ya Uchaguzi yaliyoandaliwa na Afisi ya Tume katika Ukumbi wake uliopo Maisara Jijini Zanzibar.

Mkurugenzi Khamis alisema, inapendeza Mtumishi wa Umma kuzijua Sheria, Kanuni, Sera na Miongozo ambayo inasimamiwa na Taasisi yake kulingana na Majukumu yake ili kumfanya ajiamini katika kutekeleza majukumu hayo.

Alifafanua kuwa, Afisi ya Tume imejiwekea Mkakati wa Mafunzo elekezi na endelevu kwa Watendaji wake ili kumuwezesha kila mmoja kuyajua majukumu yote ya Tume ambayo yameelezwa katika Sheria za Uchaguzi pamoja na Sheria nyengine ikiwemo Sheria ya Kuanzishwa Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 1 ya Mwaka 2017.

Akiwasilisha mada kuhusu Mzunguko wa Uchaguzi, Mkuu wa Kurugenzi ya Mipango, Utumishi na Utawala Saadun Ahmed Khamis alieleza kuwa, Uchaguzi ni Mchakato ambao unajumuisha matukio mengi ndani ya kipindi cha miaka mitano nchini Tanzania, hivyo, kumalizika kwa Uchaguzi mmoja huwafanya Watendaji wa Tume kuingia katika awamu nyengine ya Mzunguuko wa Uchaguzi mwengine.

Ndugu Saaduni alifafanua kuwa, mzunguuko wa Uchaguzi (Electoral Cycle) inatofautiana kwa mujibu wa Katiba za Nchi ambapo kwa Mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Mzunguuko wa Uchaguzi nchini Tanzania ni Mchakato wa Miaka mitano ambao hujumuisha awamu tatu za Mzunguuko huo yaani kabla, wakati na baada ya Uchaguzi.

Wakati huo huo, Mkuu wa Kurugenzi ya huduma za Uchaguzi Khamis Issa Khamis na Mkuu wa Kurugenzi wa huduma za Sheria Maulid Ame Muhammed wote kutoka Tume ya Uchaguzi walieleza kuwa, Uchaguzi ni mchakato unaoendeshwa kwa mujibu wa Sheria hivyo, ni vyema kila mdau wa Uchaguzi kuvijua vifungu vyote vya Sheria ili kuendana na misingi ya uendeshaji wa Uchaguzi.

Kwa upande wao watendaji wa Tume ya Uchaguzi wameushukuru uongozi wa Tume kwa kuona haja ya kuendesha mafunzo ambayo yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na  kwa mujibu wa Sheria na utaalamu na kujiandaa vyema na Uchaguzi wa mwaka 2025.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii