Na Jaala Makame Haji= ZEC

Walimu wa Skuli za Sekondari wameshauriwa kuwapatia wanafunzi elimu juu ya Masuala ya Kiuchaguzi ambayo itawasaidia kushiriki vyema katika chaguzi za Kitaifa wakati wanapofikia Umri wa kupiga Kura.

Ushauri huo ulitolewa na Maafisa kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika Skuli ya Sekondari ya Fuoni wakati walipofika kutoa elimu ya Wapiga Kura ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali ya Wanafunzi wa Skuli hiyo.

Maafisa hao walisema, endapo Elimu hiyo itatolewa ipasavyo kwa Wanafunzi ambao wanakaribia kutimia Umri wa Kupiga kura itachangia maendeleo makubwa ya Uchaguzi wa Kidemokrasia kwa kupunguza makosa ya kiuchaguzi na kuondosha idadi ya kura zilizoharibika.

Aidha, waliahidi kuwa kwa upande wa Tume ya uchaguzi ipo tayari kushirikiana na Walimu pamoja na Serikali za Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na Taasisi za Elimu ya juu kutoa elimu juu ya masuala ya Uchaguzi muda wowote taasisi inatakapohitaji kufanya hivyo.

Ndugu Moh’d Mrisho Yussuf mwalim Mlezi wa Serikali ya wanafunzi kutoka Skuli ya Sekondari ya Fuoni aliwashauri walimu wa Skuli za Sekondari kuwafundisha Wanafunzi masuala ya Siasa ikiwa ni miongoni mwa elimu zitakazowasaidia kuishi vyema na jamii pamoja kuwa viongozi wazuri wa Taifa.

Naye Msimamizi wa Uchaguzi wa kumchagua Rais wa Serikali ya Wanafunzi Skuli ya Sekondari ya Fuoni Moh’d Said Moh’d aliushukuru uongozi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuwapatia vifaa vya Uchaguzi pamoja na kuwapatia elimu ambayo ilihusiana na jinsi Uchaguzi wa Zanzibar unavyoendeshwa.

Kwa upande wake Mgombea wa nafasi ya Urais wa Serikali ya Wanafunzi Jeremiya Fransisiko Majaliwa, naye aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwapa elimu bora yenye manufaa ya baadaye ambayo itawasaidia kuchagua viongozi wan chi muda utakapofika.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii