Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC imemteua Mheshimiwa Jaji Aziza Iddi Suweid kuwa Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa ibara ya 119(2)(b) cha Katiba ya Zanzibar ambacho kimeipa mamlaka Tume ya Uchaguzi katika kikao cha kwanza kuteua Makamo Mwenyekiti miongoni mwa Wajumbe walioteuliwa na Rais.
Jaji Aziza Iddi Suweid ni miongoni mwa wajumbe Sita walioteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tarehe 24 Agosti, 2023 na kuapishwa leo tarehe 28 Agosti, 2023.
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imefanya kikao chake cha kwanza leo tarehe 28 Agosti, 2023 katika Afisi za Tume hiyo Maisara Mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Mheshiwa Jaji George Joseph Kazi.