Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetengua uamuzi wa kumtengua Mgombea wa Chama cha ACT Wazalendo kwa nafasi ya Uwakilishi  kwa Chama hicho ndugu.Mohammed Ali Suleiman  katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe.

Akitoa  taarifa ya maamuzi ya rufaa kwa Vyombo vya Habari katika Afisi ndogo ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar iliyopo Chakechake kusini Pemba tarehe 10 Oktoba 2023, baada ya  Chama cha ACT Wazalendo kukata rufaa kwa Tume hiyo,  Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndugu.Thabit Idarous Faina amesema,

“katika  hatua za Uteuzi wa Wagombea Uchaguzi wa Jimbo la Mtambwe, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mtambwe alipokea pingamizi mbili (2) zilizowekwa na Wagombeawa CCM na ACT Wazalendo Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi katika pingamizi hizo ulikuwa kama ifuatavyo,alimteuwa Mgombea wa CCM kwa kuamini kuwa ana sifa zote za kuteuliwa kisheria kuwa Mgombea na hakumteua mgombea wa ACT Wazalendo baada ya kujiridhisha kwamba hakutimi za sifa za kuteuliwa  kwa mujibu masharti ya kifungu  cha 51 (1) Sheria ya Uchaguzi Namba 4 ya mwaka 2018,Kufuatia uamuzi huo Mgombea wa ACT Wazalendo Ndg. Mohammed Ali Suleiman amekata Rufaa kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar  kwa kufuata masharti ya kifungu Nam 52 (1) cha Sheria ya Uchaguzi Nam 4 ya mwaka 2018”

Akielezea uamuzi wa rufaa hiyo baada ya kuzijadili hoja za utenguzi kwa pande zote mbili Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Zanzibar alisema

“Kuhusu Rufaa ya kupinga Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kumtengua Mgombea wa CCM Ndg Hamad Khamis Hamad  kuwa Mgombea kwa  sababu ya kutokukamilisha Fomu ya Uteuzi  katika Kiambatanisho cha Fomu  ya wadhamini ambayo ilijenga hoja ya kuwa taarifa zake haziwezi kumtambua Mgombea chini ya kifungu cha 51 (1) (a) Tume imeamua kwamba Msimamiziwa Uchaguzi alishindwa kuzingatia Kanuni    ya 13 (8) ya kanuni za Uchaguzi  ya mwaka 2020 ambayo inamtaka msimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha kwamba Fomu anayopokea iwe imejazwa kwa ukamilifu kwa kuwa Msimamizi alishindwa kuzingatia matakwa ya Kanuni hiyo, halikuwa kosa la Mgombea  kwa hivyo Tume ya Uchaguzi imetupilia mbali Rufaa hiyo na kuthibitisha kuwa Ndg Hamad Khamis Hamad anazo sifa za kugombea katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe”

Sambamba na hilo ameongeza kuwa kuhusu Rufaa ya kutoteuliwa kuwa Mgombea wa  ACT Wazalendo  Mohammed Ali Suleiman, kwa kutoa taarifa za uongo katika Fomu ya Uteuzi chini ya kifungu cha 51 (1) (b), Tume imebaini kuwa ushahidi uliowasilishwa kujenga hoja hiyo haukujitosheleza na hivyo imetengua uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi na kumteua Mohammed Ali Suleiman wa Chama cha  ACT Wazalendo kuwa Mgombea wa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe kupitia Chama  hicho

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mtambwe unatarajia kufanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu ambapo vyama vinne vya Siasa ambavyo ni ACT Wazalendo, Chama cha Wananchi CUF,Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHAUMMA vimeteuliwa kushiriki katika Uchaguzi huo.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii