Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar ndugu.Thabit Idarous Faina amewataka Wasaidizi Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe kufuata kanuni na sheria za Uchaguzi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu kwa watendaji wa Vituo vya Kupiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe, mafunzo ambayo yamefanyika katika Skuli ya Sekondari ya Mitiulaya iliyopo Wete Kaskazini Pemba.
Amesema Jimbo la Mtambwe linawapiga Kura wapatao elfu sita na tisini na nane na Uchaguzi ni zoezi la siku moja lenye maandalizi ya muda mrefu ambayo yanalengo la kuwaweka tayari watendaji hivyo ni vyema kutotokea kwa makosa ya Kiubinaadam kwani athari zake ni pana na kama kuna jambo ambalo watakalolihitaji ufafanuzi kabla ya uzoezi la Uchaguzi ni wajibu kuuliza kwani ni katika namna bora ya kujifunza.
Akitoa salamu za Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar amesema, Tume ya Uchaguzi Zanzibar inataka kuona kila mtendaji anafuata sheria za Uchaguzi lakini pia wasimamizi wasaidizi wanapaswa kuwa na huduma nzuri ili huduma inayotolewa katika zoezi la kupiga kura iwe huduma bora kuliko huduma nyengine.
Akiendelea kutoa salamu za Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndugu.Thabit Idarous Faina amesema, Mwenyekiti wa Tume hiyo, anawasisitiza kuwa na busara kwani watakutana na Wapiga kura wa namna tofauti na wenye nia za tofauti hivyo ni vyema kuwa makini katika kufanya maamuzi,amesema wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wanapaswa kuifuata njia nzuri ya mawasiliano ili kazi hiyo ifanyike kitaalamu.
Aidha,amesema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya juhudi kutafuta tiba ya namna ya kuyapokea matokeo kwa anaeshinda na anaeshindwa kwani kutokuwa tayari kuyapokea matokeo kwa wagombea kunaweza kuleta changamoto hiyo, hata hivyo changamoto kuyapokea matokea haiikabili tu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar bali ni Tume zote ulimwenguni.
Mkurugenzi Faina Ametoa wito kwa wasaidizi hao kuwa waadilifu na kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo,kwani ni busara kumaliza Uchaguzi na kuiacha Mtambwe na amani kama ilivyokuwa.
Aidha amewakumbusha Wasaidizi wasimamizi wa vituo vya kupiga kura kufika vituoni mapema ili kuhakikisha zoezi hilo linaanza kama lilivyopangwa na suala la ufungaji vituo liwe ni lenye kuzingatia wakati,
amesema Uchaguzi uliopita Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imepata sifa ya kutoa matokeo mapema na ndio dhamira ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutoa matokeo ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mtambwe mapema.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mtambwe utafanyika tarehe 28 Oktoba 2023.