Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mtambwe Ndugu.Othman Khamis Othman amemtangaza Mohammed Ali Suleiman wa Chama cha ACT Wazalendo kuwa mshindi wa kiti cha Uwakilishi wa Jimbo la Mtambwe katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Mtambwe baada ya Mgombea huyo kupata kura 2,449 kati ya kura 4045 halali zote zilizopigwa kwenye Shehia tano na vituo sita vya kupiga kura.
Ndugu.Mohammed Ali Suleiman amewashinda wagombea watatu kutoka Vyama vitatu vya Siasa ambao waliteuliwa kwenye Uchaguzi huo Mdogo uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2023.
Akitoa taarifa ya matokeo ya Uchaguzi huo Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mtambwe katika zoezi la majumuisho katika Ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali uliopo Daya katika Jimbo la Mtambwe, amesemaWapiga Kura walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la WapigaKura Jimbo la Mtambwe ni 6,098 ambapo kati yao 4200 ndio waliopiga kura na kura halali ni 4045 na Kura 155 zilizoharibika.
Akisoma kifungu cha 93 (6) A cha Sheria namba 4 ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 amemtangaza Mohammed Ali Suleiman kuwa mshindi wa Uchaguzi huo.
Wengine waliokuwa wanagombea nafasi ya Uwakilishi kwenye Jimbo hilo na idadi ya kura walizopata ni Mohammed Masoud Rashid wa Chama cha CHAUMMA amepata kura 22, Hamad Khamis Hamad wa Chama cha (CCM)amepata kura 1531 na Said Nassor Hemed wa Chama cha Wananchi CUF ambaea mepata kura 43.
Sambamba na uchaguzi huo wa Jimbo la Mtambwe, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imefanya Uchaguzi Mdogo Wadi ya Welezo ambapo matokeo yalitangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Wadi ya Welezo ndugu.Suleiman Hassan Haji ambapo alimtangaza ndugu.Abdul-rahman Hassan Shaaban wa Chama cha Mapinduzi (CCM)ambae ameshinda kwa kura 3,143 akifuatiwa na ndugu.Omar Shaaban Dafa wa Chama cha Demokrasia Makini ambae amepata kura 136 na Mohammed R. Vuai wa UPDP ambae amepata kura 166.
Uchaguzi Mdogo wa tarehe 28 Oktoba 2023 na kwa Jimbo la Mtambwe umefanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Habib Mohammed Ali wa Chama cha ACT Wazalendo na Wadi ya Welezo Uchaguzi umefanyika kufuatia kifo cha Diwani wa Wadi hiyo Ramadhan Ali Juma.