Tume ya Uchaguzi Zanzibar imetangaza tarehe ya kuanza zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kwa awamu ya kwanza Unguja na Pemba ambapo wapiga kura wapya wapatao 162,606 wanatarajiwa kuandikishwa.

Ameyasema hayo Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jaji George J. Kazi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa  Uchaguzi kuhusu zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura wapya kwa mwaka wa 2023 katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil uliopo kikwajuni Mjini Unguja,

Amesema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imepanga kuandikisha apiga kura wapya katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuanzia tarehe 02 Disemba  na kumaliza tarehe 15 Januari 2024, kazi hii inafanyika ikiwa  ni sehemu ya matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Pia  Tume inawajuilisha wananchi kuwa Uandikishaji huu ni wa awamu ya kwanza kutakuwa na Uandikishaji wa awamu ya pili mwanzoni mwa mwaka wa uchaguzi 2025.

 

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar amesema Uandikishaji huu utawahusu wapiga kura wapya tu ambao kimsingi hawajawahi kuandikishwa katika Daftari la kudumu la wapiga kura na wapiga kura  hao watatakiwa kwenda vituoni na vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi vilivyohakikiwa.

Akiwasilisha mada katika Mkutano huo Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndugu.Thabit Idarous Faina amesema  makadirio ya Uandikishaji wa Wapiga kura wapya Tume inakadiria kuandikisha wapiga kura wapya wapatao 162,606 kutokana na makadirio ya takwimu ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Mkurugenzi Faina amesema malengo ya zoezi hilo la kuendeleza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kuhamisha taarifa za Wapiga Kura kutoka eneo moja na kwenda jengine la kupiga kura, kusahihisha taarifa za Wapiga Kura, kuwasilisha maombi ya kuwafuta Wapiga Kura waliopoteza sifa na kuwasilisha maombi ya kitambulisho kilichopotea au kuharibika.

Sambamba na hilo amewasisitiza wananchi,kwa kila mwananchi anaeomba kuandikishwa afike katika kituo anachoomba kuandikishwa na endapo muombaji hatofika katika kituo hatoandikishwa.

Akitoa muongozo wa Kisheria katika zoezi hilo la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya Mkuu wa Kurugenzi ya Huduma za Sheria  Tume ya Uchunguzi  ya Zanzibar ndugu.Maulid Ame Mohammed ametaja miongozo na kanuni mbali mbali inayoeleza kwa undani utaratibu mzima wa uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuweka fomu mbalimbali zinazotumika katika zoezi la Uandikishaji na Uendelezaji wa Daftari kama zinavyoelezwa, amesema “Katika kufanikisha kazi za Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hutayarisha na kutoa Miongozo na Maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa kazi za Uchaguzi na utekelezaji mzuri wa majukumu ya kazi ya Uandikishaji, Miongozo na Maelekezo ya Tume itachukuliwa kuwa ni Miongozo halali iwapo tu imetiwa saini na Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Katika Uendelezaji wa Daftari, Sheria ya Uchaguzi, Kanuni za Uendelezaji wa Daftari, Maelekezo na Miongozo ya Tume ndio zana hasa zinazotumika kufanikisha kazi hii”

Akitoa Shukrani kwa niaba ya wadau wote Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ,Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud ameishukuru Tume ya uchaguzi  ya Zanzibar kwa kuweza kuwashirikisha na kuwapatia elimu hiyo ili kuweza kuwahamasisha Wananchi wenye sifa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Zoezi la Uandikishaji Wapiga kura Wapya litaanza katika kisiwa cha Pemba Wilaya ya Micheweni kuanzia tarehe 2 Disemba 2023 na kumalizia Wilaya ya Mkoani  tarehe 14 Disemba 2023 na kwa upande wa Unguja Uandikishaji utafanyika kuanzia tarehe 23 Disemba 2023 Wilaya ya Kaskazini ``A`` na kumalizika tarehe 15 Januari  2024 Wilaya Mjini.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii