Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imefunga mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa Uandikishaji watakaowafundisha Makarani watakaoteliwa na Tume kusimamia zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya katika Wilaya zote za Unguja na Pemba ambalo linatarajiwa kuanza tarehe 2 Disemba mwaka huu.

Akifunga mafunzo hayo katika Ukumbi wa Afisi ya Tume Maisara Mjini Zanzibar, Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jaji Aziza Iddi Suwedi aliwashauri Maafisa Uandikishaji kufuata Sheria, miongozo na maelekezo iliyotolewa na Tume kwaajili ya utekelezaji mzuri wa jukumu la kuandikisha Wapiga Kura Wapya katika Daftari la kudumu la Wapiga Kura.

Mhe.Aziza aliwaomba Maafisa Uandikishaji wa Wilaya pamoja na Makarani watakaoteuliwa na Tume kusimamia zoezi la Uandikishaji vituo nikuacha kabisa kusikiliza miongozo inayotokana na Wanasiasa iliyotaliwa na utashi wa kisiasa badala ya kufuata matakwa ya Sheria na Kanuni za uandikishaji.

Aidha,Jaji Aziza aliendelea kuwasisitiza Maafisa hao juu ya suala la kutunza siri za kazi lakini pia kuzingatia na kufuata mtiririko mzuri wa mawasiliano baina ya mtendaji na mtendaji kulingana na Wadhifa walionao.

“Si vyema na haipendezi kwa Afisa wa Tume kuwa na mawasiliano ya kazi na mtu wa nje bila ya kupata idhini kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi ama kupokea maagizo kwa mtu mwengine kumkiuka Mkuu wake wa kazi” alisema.

Sambamba na hilo, Jaji.Aziza aliwashauri Maafisa Uandikishaji wa Wilaya kutengeneza mtandao mzuri wa mawasiliano na kufanya kazi kwa pamoja (team work) ili kupata urahisi wa kutatua changamoto ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Nae Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabit Idarous Faina alieleza kuwa dhumuni kubwa la Mafunzo hayo nikuwafundisha Maafisa Uandikishaji wa Wilaya ili wawafundishe Makarani Uandikishaji watakaoteuliwa na Tume ya Uchaguzi kuandikisha Wapiga Kura katika Vituo vyote vya Uandikishaji Unguja na Pemba.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamewashirikisha Maafisa Uandikishaji kumi na moja wa Wilaya zote za Unguja na Pemba na yalianza tarehe 15 hadi 17 Novemba, 2023.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii