Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Thabit Idarous Faina, amesema zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya kwa Wilaya ya Micheweni limekwenda vizuri katika siku zote tatu zilizowekwa.

Aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea vituo vya Uandikishaji katika Wilaya ya Micheweni.

 “Changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwenye teknolojia zilitatuliwa kwa wakati, kupitia wataalamu wa mifumo ya Tehama, zaidi kwenye uingizaji

wa alama za vidole (Biometric),”alisema.

Aidha aliwataka wananchi wanaofika katika vituo ambapo baadhi yao alama za vidole vinaposhindwa kusoma, kuhakikisha wanasikiliza maelezo kutoka kwa Waandikishaji  ili kupatiwa haki yao ya msingi ya kuandikishwa.

Hata hivyo alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imevitembelea vituo vyote 25 ndani ya Wilaya ya Micheweni, ili kuona changamoto zinazojitokeza ndani ya Wilaya hiyo hazijitokezi katika vituo vyengine.

Nae Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe.Ayoub Bakar Hamad, alisema wananchi wamejitokeza kuandikishwa kama walivyotarajiwa na wamefurahishwa na huduma hiyo licha ya changamoto ya mifumo iliyokuwa ikijitokeza.

Aliwataka wananchi kuhakikisha wanahifadhi risiti zao ambazo wamepatiwa, ili baadae watakapotangaziwa kwenda kuchukuwa vitambulisho vyao kwenda na risiti hizo.

Alisema matarajio ya Tume ni kuandikisha tena wananchi kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025, hivyo aliwataka wananchi ambao hawakubahatika kwa awamu hii ya kwanza basi wataandikishwa tena katika awamu ya pili ya zoezi hilo.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Sizini Suleiman Shaame Hamad, alisema zoezi limekwenda vizuri katika Shehia yake, kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuandikishwa wapya.

Nae Sheha wa Shehia ya Shumba Viamboni Time Said Omar, alisema mwamko katika Shehia yake ni mkubwa licha ya udogo wa Shehia hiyo na wananchi wanajitokeza kujiandikisha.

Kwa upande wa Mawakala wa Vyama vya Siasa walisema wanashirikiana vizuri na Wakuu wa Vituo pamoja na Makarani wa vituo, ili kuhakikisha wananchi wenye sifa wanapata haki zao za kuandikishwa bila ya matatizo.

Nao Wakuu wa Vituo na Makarani wa zoezi hilo kwa Wilaya ya Micheweni kwa pamoja walisema zoezi linakwenda vizuri na wananchi wenye sifa ya kuandikishwa wanapatiwa haki  zao za kuandikishwa bila ya changamoto zozote.

Zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya wenye sifa za kuandikishwa kwa Wilaya ya Micheweni limemalizika rasmi na sasa zoezi hilo litaendelea kwa Wilaya ya Wete kwa muda wa siku tatu.

 

                                             

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii