Wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi yaZanzibar (ZEC) wamesisitizwa kuendeleza ushirikiano utakaowezesha kupata heshima katika Umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika (ECF-SADC).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jaji George J. Kazi, alieleza hayo katika hafla ya kukabidhi Tuzo kwa familia ya marehemu Hassan Said Mzee aliyekuwa Mjumbe na Makamu Mwenyekitii wa Tume hiyo, Tuzo ambazo zilizotolewa na umoja wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Kusini mwa Afrika (ECF-SADC) hafla iliyofanyika katika wa Tume hiyo.

Alisema ZEC ni moja ya Tume inayothaminiwa na kutambulika mchango wake katika Umoja huo ambapo yote hayo yanatokana na juhudi na mashirikiano waliyonayo na Serikali kuhakikisha ZEC inakuwa ni sehemu ya jumuiya za kikanda na  kimataifa zinazoshughulika na masuala ya Tume za uchaguzi.

Alisema ZEC imepata heshima kubwa ya kupata Tuzo hizo kwa kuonesha mchango wao katika kushiriki katika Jumuiya hiyo na ishara kwamba,kazi kubwa iliyofanyika kutoka kwa Marehemu Hassan Said.

Hivyo aliwataka wafanyakazi hao kuendeleza ari yao ya kufanya kazi kwa mashirikiano ya kutoa michango mbalimbali katika Jumuiya za kikanda ambazo zinatoa mafanikio ambayo yanawajenga zaidi kwa Tume hiyo na Zanzibar kwa ujumla.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi Dk. Islam Seif Salim, aliipongeza ZEC kwa kupata Tuzo hizo kwani Tuzo hiyo ni uthibitisho tosha ya kufanya kazi nzuri na kwa uadilifu katika kuiendesha Tume hiyo.

Mapema Mkurugenzi wa Tume hiyo Thabit Idarous Faina akitoa maelezo mafupi kuhusu Umoja huo alisema  unazijumuisha Tume za Uchaguzi zilizopo katika nchi za SADC ambao una wanachama 15 zikiwemo nchi za Angola, Botswana, DRC Congo na Eswatini (Swaziland).

Nchi nyengine ni Lesotho, Malawi, Mauritius, Mozambique, Namibia, South Africa, Seychelles, Tanzania bara, Zambia, Zanzibar na Zimbabwe ambapo madhumuni ya Umoja huo ni kukuza mashirikiano katika kuendesha Chaguzi za kidemokrasia ndani ya ukanda wa nchi za SADC.

Mkurugenzi Thabit alisema zipo faida zinazopatikana kutokana na kujiunga na Umoja huo ikiwemo nchi wanachama hupata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali za uchaguzi kutokana na kubadilishana uzoefu wa chaguzi wanazoziendesha nchini mwao kwa kuainisha changamoto na mafanikio yanayotokana na umoja huo.

Mafanikio mengine alisema ni kuanzishwa muongozo wa misingi ya uangalizi wa Uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya nchi za SADC ambao hutumiwa kama ni nyenzo ya Uchaguzi kwa makundi ya wanaagalizi wa Uchaguzi kikanda na kimataifa na mafanikio mengine.

Hata hivyo alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo umoja unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kutofautiana kwa muundo ya kitaasisi na mifumo ya Uchaguzi miongoni mwa wanachama katika kuendesha Chaguzi za nchi kusika.

Alifahamisha kuwa pamoja na changamoto hizo lakini ECF-SADC imefanikiwa kukuza ufanisi katika shughuli zake, kuweka mifumo mizuri ya kisheria inayohusu uchaguzi na kusaidia Tume za nchi wanachama kuendesha chaguzi zake kwa amani na kupunguza migogoro ya kiuchaguzi hasa baada ya kutangazwa kwa matokeo. 

Akizungumzia Tuzo ya marehemu Hassan Said Mzee Mkuu wa Kurugenzi ya Mipango Utawala na Utumishi Saadun Ahmed Khamis, alisema marehemu Hassan alikuwa ni mmoja wa wajumbe walioshiriki kuandaa katiba ya umoja huo na baadae kuweka saini katika katiba hiyo kwa niaba ya ZEC ambayo hadi sasa ndio inayosimamia uendeshaji wa umoja huo na kufanikiwa kupewa Tuzo  katika sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya umoja huo. 

 

“ECF-SADC imekabidhi Tuzo hii ikiwa ni kumbukumbu na shukran ya kutambua mchango wake mkubwa aliutoa wakati wa uhai wake katika kuimarisha masuala ya kidemokrasia na kuendesha uchaguzi,” alisema.

Akizungumzia Tuzo ya ZEC alisema inatokana na mchango wake inaoutoa katika umoja huo ikiwemo kuchangia mambo mbalimbali kwa kupeleka watendaji wake kusaidia shughuli za umoja.   

Akitoa neno la Shukran Jaji Said Hassan Said kwa niaba ya marehemu baba yake alipongeza Jumuiya hiyo kwa kukumbuka mchango wa watu waliosaidia katika umoja huo.

Aliipongeza ZEC kumpa heshima mzee wao kwani miaka 20 iliyopita alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa ZEC na wameona ipo haja ya kumpa heshima yake na anaamini huko alipo pia anawashikuru.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii