Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewaasa Wakuu wa Vituo na Makarani wa Uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kujiepusha na ushabiki wa kisiasa katika kipindi chote cha Uandikishaji wa Daftari hilo.

Mkurugenzi wa ZEC Thabit Idarous Faina alieleza hayo wakati akifungua Mafunzo kwa Wakuu wa Vituo na Makarani wa Uandikishaji wa Wapiga Kura katika ukumbi wa Skuli ya Dk. Ali Mohammed Shein iliyopo Rahaleo,Mjini Unguja

.

Alisema kufanya hivyo kunaweza kulitia dosari zoezi hilo hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanafanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa.

Aidha aliwasisitiza kufanya kazi kizalendo na kushirikiana hali itakayosaidia Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi hasa wakati huu wa kazi ya Uandikishaji wa Wapiga Kura.

“ZEC imewachagua nyinyi kwa kigezo cha kuwaamini kuwa mnaweza kuteleleza jukumu hili kwa ufanisi wa hali ya juu,” alisema.

Mkurugenzi Faina alisema ni vyema kwa Makarani hao kuzingatia haki ili kuona kila mwenye sifa ya kuandikishwa basi anapatiwa haki yake hiyo kwa mujibu wa Sheria bila ya kujali Chama cha Kisiasa anachotoka.

Hata hivyo, aliwasisitiza watendaji hao kutofuata maelekezo kutoka sehemu yoyote nje ya ZEC na atakaebainika kufanya hivyo hatosita kuchukuliwa hatua.

Mbali na hayo, aliwataka kuacha kutumia vifaa kwa kazi zisizohusika na kuvitunza huku akiwaasa Wakuu wa Vituo kuhakikisha wanafuata Sheria ili kuona kila mwenye haki anaandikishwa na anaepigwa kituoni anapewa haki yake ya fomu ya pingamizi.

Mbali na hayo aliwaasa kushirikiana na Masheha na Mawakala wa Vyama vya Siasa kwani jambo hilo lina umuhimu mkubwa katika kufanikisha kazi hiyo na kutunza siri kwa mujibu wa kanuni za maadili ya Utumishi wa Umma.

Mkurugenzi Faina, aliwataka Waandikishaji hao pia kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalum waliwemo Watu wenye Ulemavu, Wajawazito, Wanaonyoyesha na Watu Wazima kwani makundi hayo yanapaswa kuzingatiwa.

Akitoa mada ya maelekezo kwa Makarani wa Uandikishaji wa Wapiga Kura Msaidizi Afisa Uandikishaji Magharibi ‘B’ Maulid Suleiman Ali alisema kwa mujibu wa kifungu cha 12 (1) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 kimefafanua sifa za mtu kuweza kuandikishwa kuwa Mpiga Kura.

Akizitaja sifa hizo alisema awe Mzanzibari, awe amefikia umri wa miaka 18, awe ana kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi na kukionyesha, awe Mkaazi wa Kudumu na anaishi katika Jimbo husika kwa kipindi cha miezi 36 mfululizo lakini hatozuiwa kuandikishwa kuwa Mpiga Kura na Sheria nyengine yoyote.

Alisema karani wa Uandikishaji ni Mtendaji aliyeteuliwa na Afisa wa Uandikishaji kusimamia majukumu ya Uandikishaji katika kituo kwa mujibu wa kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.

Msaidizi Maulid alifahamisha kuwa Karani wa Uandikishaji ndiye mwenye dhamana wa kituo na atawajibika kutoa uamuzi wa Kisheria unaohusu kazi ya Uandikishaji na kazi yake ni kuwahoji Wapiga Kura watakaoingia kituoni na kutoa uamuzi unaofaa kwa waombaji kwa mujibu wa maelekezo ya Sheria.

Hata hivyo, alibainisha kuwa Karani wa Uandikishaji atakuwa na jukumu la kuwaandikisha Wapiga Kura Wapya wenye sifa wakaofika kituoni kwa ajili ya kuomba kuandikishwa na majukumu mengine wakati wote anapokuwa kituoni hapo.    

Wakizungumza kwa niaba ya makarani wenzao Catherina Paskal Mgoli  na Salum Abdul- Rahman,waliahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa kufanya kazi waliyopewa na Serikali kuona kazi hiyo inafanyika kwa ufanisi mkubwa.

“Serikali imetuamini hivyo ni vyema kwa Makarani wenzetu kwenda kufanya kazi tuliyopewa na Tume na Serikali kwa ujumla na naamini hatutakwenda kinyume na maagizo tuliyopewa ili kuweza kuwasaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kuona wanapata haki yao ya msingi,” walisema.    

Naye Mkuu wa kituo cha Uandikishaji Ali Hassan Khamis aliahidi kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na ushirikiano ili kuleta ufanisi katika Daftari hilo na kuahidi kutokwenda kinyume na matakwa aliyopewa na ZEC.

Aliwaomba Wakuu wa Vituo kushirikiana pamoja ili kuona wanafanikisha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa na kuwasisitiza wananchi wote ambao wenye sifa ya kuandikishwa basi kujitokeza kutumia haki yao hiyo.

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii