Wanasiasa watakiwa kubadilika na kuwa wakweli  ili kuepuka kuopotosha Umma

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji George J. Kazi amewataka Wanasiasa kubadilika na kuwa wakweli wanapoeleza  shughuli zinazofanywa na Tume hiyo ili kuepusha siasa za Uchochezi na hatimae kuibakisha nchi ikiwa salama.

Alisema kuendelea kuwapa habari wananchi zisizo na ukweli ni sawa na upotoshaji kwani mambo yote yanayoendeswa na Tume hayafichwi yako wazi na kila mmoja anaona na wadau mbali mbali wamekuwa wakishirikishwa katika kazi za ZEC ikiwemo Uandikishaji Wapiga Kura.

Jaji Kazi, alieleza hayo huko katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake Chake Pemba katika Mkutano wa Tathmini ya zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya kwenye Daftari la kudumu  lililoendeshwa na Tume hiyo kwa Mikoa yote ya Zanzibar kuanzia tarehe  2 Disemba  2023 hadi tarehe 15 Januari 2024.

Alisema kuwa wakati wa Zoezi la Uandikishaji likiendeshwa viongozi wote wa Tume hiyo walikuwa wakifuatilia na kulikuwa na mashirikiano makubwa baina ya watendaji na Mawakala wa Vyama vya Siasa ,hivyo dosari yoyote ilikuwa inajitokeza ilikuwa inapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake hiyo.

“ Watendaji wote wa Tume hii walikuwa hawakai Ofisini kuanzia mwanzo wa zoezi mpaka mwisho wa zoezi hivyo changamoto zote ambazo zilikuwa zinajitokeza katika zoezi hilo zilipatiwa ufumbuzi wa pamoja na nichukuwe fursa hii kuwapongeza wadau wote kwa ushirikiano wenu mulioipatia Tume yetu”, alisema.

 

 

Akizungumzia kumalizika kwa zoezi hilo Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa zoezi lilikwenda vyema kwa Amani na utulivu.

Alisema katika zoezi hilo jumla ya Wapiga Kura Wapya  57,883wameandikishwa wakiwemo Wanawake 31,440 na Wanaume 26,443 sawa asilimia 35.6 ya walioandikishwa ingawaje matarajio ni kuandikisha Wapiga Kura Wapya 162,606, lakini pamoja na zoezi hilo kumalizika kazi inayofuata ni kuweka wazi Daftari kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 1 hadi 7 Machi 2024.

Aliwataka Wadau wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kuwahamasisha Vijana waliomba kuandikishwa kwenda vituoni kuangalia taarifa zao kwani kufika kwao vituoni kuona taarifa zao kutawarahisishia nafasi ya kuwemo katika Daftari na kuwa Wapiga Kura.

“ Tume inawaomba Wananchi  muendelee kudumisha Amani na utulivu ndani ya nchi yetu na kutoa ushirikiano mzuri kwa shughuli zinazoendeshwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar katika mzunguko wote wa Uchaguzi”, alisema.

Akitoa Tathmini ya Wapiga Kura wapya awamu ya kwanza Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar , Thabit Idarous Faina alisema kuwa kifungu cha 19 ( 1) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kinaelekeza afisa Uandikishaji baada ya kukamilika kwa Uandikishaji Wapiga Kura kwa kufuata miongozo ya Tume ataweka wazi orodha ya waombaji wapya katika kila kituo cha Uandikishaji kwa muda wa siku 7.

Alifahamisha sambamba na hilo pia kifungu cha 19 (2) kinaeleza kuwa Mpiga Kura yoyote au muombaji anaweza kuchunguza orodha ya Wapiga kura  iliowekwa wazi kwa madhumuni ya kuthibitisha kuwa yumo, kuangalia usahihi wa taarifa zake au kuweka pingamizi taarifa za muombaji mwengine asiekuwa na sifa katika orodha hiyo.

Alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa mujibu wa mpango kazi wake itaendesha zoezi kama hilo kwa awamu ya pili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2025.

“ Niwahakikishie wadau Uchaguzi kuwa shuguli zote zinazofanywa na Tume hii zinakwenda kwa mujibu wa Sheria na sio kwa matakwa ya watu wengine “, alisema

Alifahamisha kuwa wakati wa zoezi hilo wadau mbali mbali walishirikishwa na Tume kuanzia ngazi ya mwanzo hadi ya mwisho kwa mujibu wa nafasi zao wakiwemo  Vyama vya Siasa, vikosi vya Ulinzi na Usalama, asasi za kijamii Vyombo vya habari , makundi maalumu nakadhalika.

Mkurugenzi huyo alisema katika kufanikisha zoezi hilo kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya mwaka 2018 , kifungu cha 14 (1) Vyama vya Siasa viliruhusiwa kuweka Mawakala wao katika vituo vyote vya Uandikishaji ili kuangalia mwenendo wa Uandikishaji ambapo jumla ya Vyama 14 viliweka Mawakala wao.

Alieleza vyama 5 vya siasa havikuweka Mawakala wao katika zoezi hilo kwa sababu zao mbali mbali, aidha asasi za kiraia 10 zilishiriki zoezi hilo .

Aliwapongeza wadau wote wa Uchaguzi kwa ushiriki wao katika kufanikisha zoezi hilo na kuwataka waendelee kudumisha Amani na utulivu kwani ndio uliowezesha kufanyika kwa kazi hiyo muhimu ya Kidemokrasia.

Nae Mkurugenzi wa Huduma za Uchaguzi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndugu Khamis Issa Khamis alisema mpaka kufikia tarehe 15 Febuari mwaka 2024 jumla ya wapigakura 323 wameshawasilisha maombi ya kuhamisha taarifa zao kutoka eneo moja kwenda jengine la Uchaguzi.

Alieleza kuwa uhamisho wa taarifa za Wapiga kura ni endelevu  na kazi ya kupokea taarifa za wanaoomba kuhamisha inaendelea kufanyika katika Afisi za Uchaguzi za Wilaya kila siku kwa saa za kazi.

Hata hivyo Tume inawasisitiza wananchi kudumisha Amani na Utulivu wakati wa zoezi la kuangalia taarifa zao sambamba na kutowa ushirikiano mkubwa ili zoezi liende vizuri.

 

           

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii