Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) imeendesha mafunzo ya siku moja ya kuwajenga uwezo na uelewa juu ya utoaji huduma wa Mfuko huo visiwani Zanzibar.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ukumbi wa Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ iliyopo Mwera nje kidogo ya jiji la Zanzibar  lengo likiwa ni kuwaandaa wadau muhimu katika  matumizi ya Mfuko huo nchini.

Akifungua mafunzo hayo Afisa Masoko na Uhusiano kutoka Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF)  Asha Kassim Mbiwi  alisema Mfuko huo umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya mwaka 2023 ambayo ni   Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar,Sheria  ambayo ina umuhimu mkubwa nchini kwani inalenga katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote za uhakika na endelevu kwa wananchi na wakaazi wote wa Zanzibar na kuhakikisha upatikanaji wa rasimali fedha za kutosha na endelevu za kugharamia huduma za afya kwa wote hatua ambayo itaweza  kuweka mazingira bora ya kukuza na kustawisha huduma za Afya nchini.

Akizungumzia baadhi ya majukumu ya Mfuko huo alisema unajikita katika kulipia huduma za Afya kwa  wanachama na wategemezi wao,kukusanya, kuhifadhi na kusimamia michango ya wanachama pamoja na fedha nyengine zitakazolipwa na kulinda maslahi ya wanachama.

 Aliwakumbusha washiriki kuyatumia vyema mafunzo hayo ili kujijengea uelewa wakutosha  na uelewa sahihi wa Mfuko huo kwani wadau mbali mbali wamekuwa na maswali mengi juu ya Mfuko huo.

“kupitia mafunzo haya mtaweza kuuliza maswali ya kina pamoja na kutoa maoni yenu muhimu kuhusu huduma hii ili tuweze kuyazingatia na kuyatekeleza kwa maslahi ya wananchi wetu hapa Zanzibar  hasa nyinyi wafanyakazi wa Serikali ambao ni miongoni mwa makundi ya kwanza kufikiwa katika elimu hii ambayo ilianza kwa ngazi za juu za viongozi wa juu wa kila Taasisi za Serikali ya Zanzibar’’ alisema.

Aidha,  alisema wataendelea na program za kutoa elimu kwa Taasisi za Serikali hadi pale watakapokamilisha kutoa mafunzo kwa Taasisi zote za Serikali na zoezi kama hilo linafanyika Unguja na Pemba na zoezi kama hili litafanyika pia kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.

Akitoa ufafanuzi juu ya maswali mbali mbali yaliyoulizwa katika mafunzo hayo Bi.Asha  alisema Mfuko huo bado haujawafikia Wazanzibar wote na umeanza kwa Wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini malengo ni kuwafikia Wazanzibar wote na Mfuko huo unaamini kuwa taarifa muhimu kuhusu huduma hiyo mpya zitawafikia walengwa wote kote nchini,

Nae Afisa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Bi Mwanamkuu Gharib Mgeni Alisema mafunzo hayo yamewapa faraja wafanyakazi wa Tume kwani wameelewa jinsi Mfuko unavyofanya kazi na walengwa wa Mfuko huo,na mafunzo hayo yamewanufaisha na kujua azma ya Serikali na muelekeo wake,amewaasa wafanyakazi kutoiacha fursa hiyo muhimu kwani huwezi kufanya kazi ukiwa huna afya bora.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mkuu wa kurugenzi ya Huduma za Sheria ndugu.Maulid   aliwashukuru na kuwapongeza kwa kuwapatia mafunzo hayo juu ya Mfuko huo.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii