Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imepongezwa kwa utoaji wa Elimu ya Wapiga Kura kwa Taasisi mbali mbali jambo ambalo linakuza Demokrasia nchini.

Pongezi hizo  zimetolewa na viongozi wa Vyuo Vikuu Tanzania  ambao ni wajumbe wa  Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO)  walipokuwa katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Jumuiya hiyo ambapo mada mbali mbali zilijadiliwa, Mkutano ambao umefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha SUZA kilichopo Tunguu Wilaya ya Kati Unguja, ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Rais wa TAHLISO uliofanyika tarehe 06 Aprili 2024.

Akitoa pongezi zake ndugu.Raifa Abdallah Makame  ambae aliteuliwa katika Mkutano huo kuwa ni Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya TAHLISO mara   baada ya kupatiwa Elimu ya Wapiga Kura alisema  katika Mkutano huo wamejifunza vitu mbali mbali ikiwemo namna ya kupiga kura pasina kuharibika lakini na kujua kanuni mbali mbali zinazomuhusu Mpiga Kura hali ambayo utaufanya Uchaguzi wa TAHLISO uwe wa huru na haki kwani kila Mpiga Kura sasa anajua haki yake katika Uchaguzi huo.

Sambamba na hilo aliwapongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kuwapatia muamko huo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri  kwa vijana wengine.

Nae Khamis Abam Dilo ambae ni mshiriki wa Mkutano huo lakini pia ni Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya TAHLISO alishukuru kuwa moja ya washiriki waliopatiwa Elimu ya Wapiga Kura kwani mafunzo hayo yamemuwezesha kujua mipaka yake katika zoezi la Uchaguzi,

Aliwaasa Wajumbe wa Mkutano huo Kupiga Kura kwa salama na amani kwani kuna maisha baada ya Uchaguzi.

Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo  ndugu.Mohammed Idrissa Haji ambae ni Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Wapiga Kura alisema lengo la kuwapatia elimu hiyo ni kuwawezesha kuwa na uelewa sahihi kuhusu zoezi la Upigaji wa Kura na kujua  Kanuni na Sheria zinazosimamia Uchaguzi ili kupunguza idadi ya Kura kuharibika katika Chaguzi mbali mbali ikiwemo zinaezoendeshwa na Taasisi za Elimu.

Aliwakumbusha Wajumbe wa Mkutano huo kuyazingatia Mafunzo kwani tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani 2025 ambapo wananchi watapata nafasi ya kuchagua viongozi mbali mbali hivyo ni vyema kuizingatia elimu hiyo.

Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha SUZA ulijumuisha Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO ambao ni Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Maspika wa Serikali za Wanafunzi nchini.

Katika Mkutano huu uliolenga kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Wanafunzi, Wadau na Wageni mbalimbali maalumu wameshiriki ikiwemo Wadau kutoka NHIF,NACTVET, HESLB, CRDB, NMB,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Wadau wa Bodi ya Mikopo kutoka Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii