Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imekamilisha zoezi la uandikishaji Wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa Wilaya ya Micheweni ambalo lilidumu kwa Siku tano katika kila kituo.

Akizungumza na Waandishi wa habari huko ofisini kwake mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Afisa uandikishaji wa Wilaya ya Micheweni Seif Salum Juma amekiri kuwa zoezi la Uandikishaji wa wapiga kura katika Wilaya hiyo lilikwenda vizuri licha ya kutangazwa kuwepo kwa dosari ambazo yeye kama msimamizi mkuu hajazipokea kutoka kwa Watendaji wake.

“Kwakweli hakukua na changamoto zozote zaidi ya hiyo na watendaji wetu tumewapa mafunzo ya kutosha hivyo wataalamu waliweza kurekebisha na zoezi liliendelea vizuri kama ilivyopangwa” alisema.

Ndugu Seif Salum alieleza kuwa, mwitikio wa wananchi katika Wilaya ya Micheweni ni mkubwa mno kwani  Tume ilikuchukua jitihada za kuwahamasisha wananchi ili waweze kujitokeza kwa wale ambao wanasifa za kujiandisha na kufanyiwa uhakiki.

Seif, alifahamisha kuwa Muda wa siku tano unatosha kuendesha zoezi la kuandikisha kutokana na mwitiko wa siku ya kwanza katika Wilaya ya Micheweni ulikuwa mkubwa lakini ikiwa leo ni siku ya mwisho ya Uandikishaji ni wachache wanaojitokeza katika vituo hivyo na pengine karani anakaa muda wa nusu saa anatokea mtu mmoja kwa baadhi ya vituo hali ambayo ni tofauti na siku za mwanzo.

Afisa Uandikishaji  (ZEC) Wilaya ya Micheweni, Seif Salum Juma,akizungumza na Waandishi wa habari katika Afisi ya Uchaguzi ya Wilaya ya Micheweni  mara baada ya kumalizika kwa zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura katika Wilaya hiyo.

 

Nae , Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba, Salama Mbarouk Khatib, alisema ni vyema Waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuripoti mambo ya msingi kuliko kutoa taarifa zisizokuwa na uhakika juu ya zoezi la Uandikishaji linalomaliza muda wake katika Wilaya hiyo.

Alieleza kuwa zoezi la Uandikishaji wa Daftari hilo lilienda vizuri na linamalizika kukiwa na amani na utulivu na hakuna dosari yoyote iliolikumba na kupelekea kutangazwa katika Vyombo vya habari kwani Wananchi wote wenye sifa walijiandikisha na kufanyiwa uhakiki na wale wachache ambao walikosa sifa walielekezwa kufuata taratibu za kisheria.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa anaipongeza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kujipanga vyema ili kukamilisha kazi zake za Uandikishaji na uhakiki kutokana na kuwapatia huduma wale wote waliokwenda vituoni kujiandikisha au kuhakiki taarifa.

Niwapongeze pia Wananchi wa Wilaya ya Micheweni kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya Uandikishaji wapiga kura na uhakiki wa taarifa zao kama ilivyokusudiwa na Tume,”alisema.

Akizungumzia suala la amani na utulivu ndani ya Wilaya hiyo liko vizuri wananchi wanafanya shughuli zao na wale wanaokwenda kutafuta haki yao hiyo ya kujiandikisha wanakwenda bila ya wasi wasi wowote kwani Wilaya imejidhatiti kwa sauala la ulinzi wa amani muda wote.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Pemba, Salama Mbarpuk Khatib, akizungumza na Waandishi wa habari juu ya zoezi la Uandikishaji wa Daftari la kudumu na uhakiki wa taarifa za wapiga kura, lililoanza Wilayani humo tarehe 18 hadi 22 /1 mwaka huu

 

Hata hivyo Mawakala wa Chama cha Siasa cha ACT –Wazalendo, Bakar Hamad Shehe wa Kituo cha Tumbe mashariki alisema zoezi la uandikishaji wa Wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura wa zamani lilikwenda vizuri

Kwa vile walitegemewa kuandikishwa na kufanyia uhakiki ni wachache nasema kuwa zoezi limekwenda vizuri na hata kama waliotakiwa wapatiwe hali hiyo walikuwa wengi basi wengefanyiwa hivyo,”alisema.

Aidha Wakala wa chama cha Siasa cha ACT Wazalendo, wa Kituo cha Tumbe Magharibi, Khamis Omar Iddi, alikiri zoezi hilo kuendeshwa vyema na wale wote ambao walijitokeza kuomba huduma hiyo walifanikiwa kupata lile walilolikusudia.

“ Mimi niseme zoezi hili limekwenda vizuri na hakuna tatizo lolote ambalo tulikutana nalo kama Mawakala , tulishirikiana vyama vyote  na kuwaelekeza wananchi kufuata taratibu za kisheria,”alieleza.

Kwa upande wake wakuu wa vituo vya Uandikishaji  Wilaya ya Micheweni, Rashid Juma Salum ,Tumbe –Magharibi na  Abdalla Yussuf Hamad,Tumbe Mashariki, walisema zoezi lilikwenda vizuri kutoka siku ya mwanzo hadi siku ya mwisho ingawaje siku hiyo ya mwisho wananchi wanaokwenda kujiandikisha sio wengi lakini wapo wanaendelea kusubiri hadi mwisho wa ufungaji wa kituo ili kuona ni watu wangapi watajitokeza.

Zoezi hilo la Uandikishaji wapiga kura na uhakiki wa taarifa za wapiga kura lilianza tarehe 18/1 na linatarajiwa  kumalizika tarehe 22/1 /2020 Kwa Wilaya ya Micheweni Pemba.

 

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii