Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar zec iliwahakikishia wananchi kuwa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura litaendeshwa kwa misingi na taratibu za kisheria zilizopo ili kila mwenye sifa anapata haki ya kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la wapiga kura

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Uchaguzi Tume ya uchaguzi ya Zanzibar SULEIMAN HASSAN HAJI wakati akifungua mkutano wa wadau wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini “A” uliofanyika katika kituo cha walimu Mkwajuni ambao umewashirikisha viongozi wa Serikali,viongozi wa Dini, vyama vya siasa, jeshi la polisi na asasi za kiraia

Afisa huyo alisema, zoezi la uandikishaji linamuhusu kila mtu aliyetimiza sifa hivyo, ni wajibu wa kila mwananchi kuzingatia maelekezo na elimu inayotolewa na Tume kwa kuhamasishana na kushiriki katika zoezi hilo linalotarajiwa kuanza tarehe 9/2/2020 kwa Wilaya  hiyo na shehia za jimbo la Donge.

Akitoa muongozo na utaratibu wa uandikishaji wa Daftari Afisa uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini “A” BAKAR BURHANI SULEIMAN amesema ili uweze kushiriki katika zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa ni lazima uwe na kitambulisho kipya cha mzanzibar mkaazi pamoja na kitambulisho cha kupigia kura kwa wapiga kura wanaohakiki taarifa zao.

Afisa Uchaguzi Wilaya Kaskazini “B” MAKAME PANDU KHAMIS alisisitiza kuwa ni vyema kuzingatia kuwa Kazi ya Uandikishaji inafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam.4 ya mwaka 2018 hivyo, ni wajibu wetu kufuata kivitendo sheria hiyo ili kuepukana na vitendo ambavyo vinaweza kusababisha fujo katika nchi yetu.

Naye Msaidizi Afisa Uchaguzi Wilaya kaskazini “B” MARYAM MAJID SULEIMAN aliwaasa wananchi kutothubutu kwa makusudi au bahati mbaya kuharibu zoezi la Uandikishaji kwani Sheria hiyo ya Uchaguzi imeweka adhabu kali kwa atakayeharibu zoezi hilo ambazo ni pamoja na kifungo kisicho pungua miezi mitatu na kisichozidi miezi sita au faini ya fedha zisizopungua laki tatu na zisizozidi milioni tatu.

Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “A” HASSAN ALI KOMBO aliwataka washiriki wa Mkutano huo kuifikisha kwa Wananchi elimu waliyopatiwa na Tume ya uchaguzi ili kila mmoja aweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujiandikisha na kuhakiki taarifa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliishauri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendelea kushirikiana na Wakala wa usajili wa matukio ya kijamii ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vipya vya mzanzibar mkaazi sambasamba na kuzingatia ushiriki wa watu wenye mahitaji maalum katika vituo vya kujiandikisha.

Afisa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini A BAKARI BURHAN SULEIMAN akiwasilisha mada katika mkutano wa Wadau wa uchaguzi Wilaya ya Kaskzini B uliofanyika SKuli ya Mahonda tarehe 29/1/2020

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii