JAALA MAKAME HAJI- ZEC

Dhana ya Ushirikishwaji wa Wadau wa Uchaguzi ni jambo linalohitaji kupewa umuhimu wa kipekee katika masuala ya kiuchaguzi ambayo hutoa fursa ya kukuza maendeleo ya demokrasia nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar THABIT IDAROUS FAINA katika ukumbi wa Haile Selassie wakati akifungua semina ya viziwi ikiwa ni muendelezo wa Tume hiyo kukutana na wadau wa Uchaguzi kwa lengo la kutoa taarifa juu ya mambo ambayo Tume inatarajia kuyafanya katikma kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mkurugenzi Faina alifahamisha kuwa, katika kufikia malengo yake Tume imeandaa kamati za ushauri ambazo miongoni mwa wajumbe wake ni kutoka taasisi za wadau wa Uchaguzi wakiwemo Vyama vya Siasa, Asasi za kiraia, Taasisi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) THABIT IDAROUS FAINA akifungua semina ya VIZIWI iliyoandaliwa na Tume hiyo katika ukumbi wa Haile Selasie tarehe 9/2/2020 Jijini Zanzibar ikiwa ni muendelezo wa Semina za Wadau wa uchaguzi kutoka Makundi Maalum katika maandalizi ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura Unguja unaotarajiwa kuanza tarehe 15/2/2020 mpaka 10/3/2020

Akizungumzia kuhusu ushauri wa wadau wa Uchaguzi juu ya matumizi ya risiti za vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi katika zoezi la Uandikishaji,  Mkuu wa Kurugenzi ya Uandikishaji na TEHAMA, MWANAKOMBO MWACHANO ABUU alisema mfumo wa mashine za kuandikishia hauwezi kusoma risiti, hivyo ni vyema wananchi kufanya juhudi ya kutafuta kitambulisho kipya cha Mzanzibari Mkaazi ili aweze kutambuliwa na kuweza kuandikishwa kupitia mfumo huo.

Mada nne ziliwasilishwa katika semina hiyo ikiwemo mada ya ushikiano wa Tume ya Uchaguzi na wadau wa Uchaguzi iliyowasilishwa na Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga kura, Habari na Uhusiano JUMA SANIFU SHEHA alisema ushirikiano wa Tume na wadau wa Uchaguzi ni sifa moja wapo ya Tume huru na ni kiashiria tosha cha kuwa na chaguzi za haki, wazi na za kuaminika.

Mwenyekiti wa chama cha viziwi Zanzibar (CHAVIZA) ASHA ALI HAJI aliiomba Tume kushirikiana na CHAVIZA ili kupata wakalimani ambao watawasaidia viziwi katika vituo vya kujiandikisha na kupigia kura.

Akifunga semina hiyo Mkuu wa Kurugenzi ya Utawala na Mipango Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar SAADUN AHMED KHAMIS alisema ushirikishwaji wa makundi maalum ni utekelezaji wa sera ya jinsia na ushirikishwaji wa makundi ya kijamii ya mwaka 2014 iliyotungwa na Tume ili kuyashirikisha makundi hayo katika harakati za kiuchaguzi.

 

Mkalimani wa Lugha ya alama kutoka Idara ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar IBRAHIM KHAMIS MWINYI akiwa mbele ya VIZIWI walioshiriki Semina ya Makundi Maalum kutoka kundi la VIZIWI iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika Ukumbi wa Haile Selasie Jijini Zanzibar tarehe 09/2/2020 kwa lengo la kutoa elimu ya Wapiga Kura juu ya Uandikishaji na Uhakiki wa Wapiga Kura unaotarajiwa kuanza tarehe 15/2/2020 mpaka tarehe 10/3/2020 Unguja. (17:09:48)

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii