Na Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) iliwataka makarani wa Uandikishaji kusimamia Sheria, Kanuni na Miongozo ya uandikishaji waliyopatiwa katika mafunzo ili kuwawezesha kutekeleza vyema majukumu yao wakati wanapokuwa katika vituo vya Uandikishaji.

Akizungumza katika mafunzo ya Siku mbili ya makarani wa Uandikishaji yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Chumbuni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo THABIT IDAROUS FAINA alisema umakini na uadilifu wa makarani hao utasaidia kupunguza malalamiko kwa Wananchi wakati wanapokwenda vituoni kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao.

Mkurugenzi FAINA aliwataka Makarani hao kushirikiana katika utendaji kazi wao na kuhakikisha wanatekeleza dhamana zao walizokabidhiwa na Tume ya Uchaguzi kwa kufanya uadilifu, usawa na uwazi ambao ndio msingi wa demokrasia katika nchi.

Mkurugenzi huyo aliwahakikishia Wananchi kuwa Tume itamuandikisha kila mwenye sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo aliwaomba Wapiga Kura waliokuwemo katika Daftari kwenda katika vituo vyao vya Kupigia Kura kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao kwani bila kufanya hivyo hawatoweza kupiga kura kwa uchaguzi ujao.

 Akiwasilisha mada katika Mafunzo hayo, Afisa Uandikishaji Wilaya ya Mjini SAFIA IDI MOHAMMED alisema, Tume itafanyakazi ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa muda wa siku tano kwa kila kituo ambapo Vituo vyote vitaanza kufunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni.

Afisa Msaidizi wa Uandikishaji Wilaya ya Magharib “A” MWANAMKUU GHARIB MGENI alisisitiza kuwa Tume itatumia kitambulisho kipya cha Mzanzibar Mkaazi badala ya kile cha Zamani na kuwataka Wananchi wanaoomba kuandikishwa kuchukuwa vitambulisho hivyo na kwa wale Wapiga Kura wa zamani watatakiwa kwenda vituoni kwa kuhakiki taarifa zao na watapaswa kuchukua vitambulisho vipya vya Mzanzibari Mkaazi pamoja na Vitambulisho vya Kupigia Kura.

Akizungumza mara baada ya mafunzo  mshiriki wa mafunzo hayo KALATHUMI KONDO MAKAME aliwaomba wananchi kushiriki kwa wingi kuandikisha na kuhakiki taarifa zao na kuwaomba wananchi hao kuondoa hofu na jazba wanapofika vituoni.

Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi ya Kijamii ya mwaka 2015 ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Bw. MUSSA HASSAN MUSSA ambaye ni mshiriki wa  mafunzo hayo alisema Tume tayari imewapatia muongozo makarani wa uandikishaji kutoa fursa maalum kwa Watu Wenye mahitaji maalum ya kutopanga foleni wakati wanapofika vituoni kujiandikisha au kuhakiki taarifa zao, watu hao ni pamoja na Watu wenye Ulemavu, wajawazito na wanaonyonyesha. 

Kazi ya uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura waliokuwemo katika Daftari Kudumu la Wapiga Kura kwa upande wa Unguja unaanza tarehe 15/2/2020 Wilaya ya Kaskazini “A” na Jimbo la Donge kwa Wilaya ya Kaskazini “B” na kumalizika tarehe 10/3/2020 katika Wilaya ya Mjini.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii