Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeanza rasmin kazi ya Uandikishaji wa Wapiga Kura wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura waliokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Wilaya ya Kaskazini “A” ambapo wananchi wa Wilaya hiyo wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kujiandikisha.

Kazi hiyo imeanza katika Shehia zote za Wilaya Kaskazini “A” na Shehia za Jimbo la Donge kwa Wilaya Kaskazini “B” ambapo Vituo vyote vilifunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi jioni.

Wakizungumza katika vituo hivyo baadhi ya wananchi wameipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuandaa mazingira mazuri huku wakiomba kuongezewa muda ili kila mwananchi aweze Kujiandikisha na kuhakiki taarifa zake

wakizungumza baada ya kupata huduma ya kuhakiki taarifa zao PAKACHA RAMADHAN na MAKAME HAJI ALI wote ni wakaazi wa Nungwi wamesema zoezi limeanza vizuri kwakuwa mfumo unaotumiwa na Tume kuandikisha na kuhakiki taarifa unatumia muda mfupi ambapo wamewaomba wananchi  kutowa wasiwasi juu ya kutumia muda mkubwa katika vituo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi THABIT IDAROUS FAINA wakati wakitembelea vituo hivyo amewataka wananchi kuutumia vizuri muda uliopangwa na Tume kwa kuwa muda huo wa siku tano ulipangwa kwa kila kituo unatosha kutokana na mfumo unaotumika kuandikisha wananchi na kuhakiki taarifa za Wapiga Kura unatumia muda mdogo sana wastan wa dakika moja mpaka mbili kwa mwananchi mmoja.

Mkurugenzi wa Uchaguzi THABIT IDAROUS FAINA (wa kati Koti jeusi) akiwa katika Kituo cha Uandikishaji cha Shehia ya Kidoti kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura iliyoanzan katika Wilaya ya Kaskazini kuanzia tarehe 15/2/2020 na kudumu katika Wilaya hiyo kwa muda wa siku tano

Mkurugenzi FAINA amesema Tume ya Uchaguzi itamuandikisha kila mwananchi aliyetimiza sifa za kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 4 ya mwaka 2018 ili kuweza kupiga kura katika Uchaaguzi Mkuu wa 2020.

Kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura waliokuwemo katika Daftari la kudumu kwa Wilaya ya Kaskazini “A”  itaendelea kwa muda siku tano katika kila  kituo kilichopangwa na Tume hiyo.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii