Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilisema baada ya zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kukamilika itafanya tathmini ili kuangalia kwa namna ambavyo itaweza kusaidia kuzitatua changamoto za Wananchi ambao watakosa fursa ya kuandikishwa katika Daftari kutokana na sababu ya kukosa Vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi wakati zoezi hilo linaendelea.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziaza ya kutembelea vituo vya uandikishaji vya Wilaya ndogo ya Tumbatu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe. Jaji Mkuu Mstaafu HAMID MAHMOUD HAMID alisema lengo la ziara hiyo ni kupata tathmini ya awali ili kujua mafanikio na changamoto juu ya utaratibu wa uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura unavyoendelea.
Mwenyekiti Hamid aliongeza kwa kusema changamoto kubwa ambayo inajitokeza katika zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura ni baadhi ya wananchi kukosa vitambulisho vya mzanzibar mkaazi ambapo amewashauri Wananchi hao kuendelea kufuatailia vitambulisho hivyo ili waweze kushiriki katika zoezi hilo linaloendelea.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (kulia) Mhe. Jaji Mkuu (mst) HAMID MAHMOUD HAMID akihoji jambo kwa wakala wa Uandikishaji Mwalim Kali Silima (kushoto) alipotembelea kituo cha uandikishaji cha Shehia ya Tumbatu Uvivini.
Baadhi ya Makarani na mawakala katika Vituo vya uandikishaji kisiwani Tumbatu waliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuweka utaratibu na mfumo mzuri wa Uandikishaji ambao umepelekea zoezi hilo kufanyika katika hali ya amani na utulivu na Wananchi wa Tumbatu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuhakiki taarifa zao.
Sheha wa Shehia ya Jongowe (aliyekaa) MIZA ALI SHARIF akimpa maelezo Maelezo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Hamid Mahmoud Hamid alipotembelea katika Kituo cha Uandikishaji cha Shehia hiyo.
Kwa nyakati mbali mbali Masheha wa Shehia wakiwa ni wakala wa Tume katika vituo vya uandikishaji walisema wananchi wengi ambao wamepata vitambulisho vya mzanzibar mkaazi tayari wameandikishwa na kuhakiki taarifa zao na kuwaomba ambao wako nje ya kisiwa kufanya jitihada ya kuandikisha kabla ya kumalizika siku tano zilizopangwa.
Mwenyekiti HAMID MAHMOUD HAMID alitembele kituo cha Tumbatu Jongowe, Uvivini, Gomani na Mtakuja na katika ziara hiyo alifatana na Kamishna wa Tume Mhe. Jaji KHAMIS RAMADHAN ABDALLA, Mkurugenzi wa Uchaguzi THABIT IDAROUS FAINA na baadhi ya watendaji wa Tume hiyo.
.