JAALA MAKAME HAJI- ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imewaomba Wapiga Kura waliomo ndani ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao muda ukifika ambapo kazi hiyo ya uhakiki itafanyika sambamba na kazi ya kuandikisha Wapiga Kura wapya katika daftari hilo kwa mujibu wa ratiba itakayotolewa na tume.

Akizungumza katika semina ya wanafunzi wa skuli za sekondari za wilaya ya Magahrib “A” Afisa Uchaguzi wa Wilaya hiyo ndugu. Ali Rashid Suluhu alisema wapiga kura wote watapaswa kuhakiki taarifa zao za kitambulisho cha mzanzibar mkaazi ambacho kitawawezesha kuhakiki taarifa zao katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwani bila kuhakiki taarifa huwezi kupiga kura kwa Uchaguzi ujao.

Akizungumzia kuhusu uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya ndugu Suluhu aliwata wazazi na walezi kuwahamasisha vijana ambao wamefikia umri wa miaka kumi nane ambao hawana vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi kufanya jitihada za makusudi kupata vitambulisho hivyo ili nawao waweze kuandikishwa kuwa Wapiga Kura muda ukifika.

Naye msaidizi Afisa uchaguzi Wilaya ya Kaskazini “A” Bi Miza Pandu Ali alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itaweka wazi majina ya wapiga kura katika vituo vyote vya kujiandikisha baada ya kumaliza kazi ya uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Bi Miza Pandu alifahamisha kwamba, lengo la kuweka wazi majina ya wapiga kura ni kuwapa fursa wapiga kura kujiridhisha kuhusu usahihi wa taarifa zao na kuweka pingamizi kwa wapiga kura ambao hawana sifa za kuandikishwa katika eneo husika.

Bi Miza aliongeza kusema kwamba, wakati wa zoezi la uandikishaji Tume haitofanya shuhuli za uendelezaji wa Daftari kwa wapiga Kura wanaoomba kubadilisha na kusahihisha taarifa zao pamoja na Wapiga Kura waliopoteza shahada zao na badala yake shuhuli hizo zitafanyika katika ofisi za Uchaguzi za Wilaya mara baada ya kukamilika kwa kazi ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi wa skuli za sekondari za Wilaya ya Magharib “A” wameiomba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendelea kutoa elimu ya Wapiga Kura ili kila mwananchi aweze kutumia haki yake ya kupiga kura muda ukifika.

Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini A Ndg. BAKAR BURHANI SULEIMAN akizungumza na wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Bububu katika mafunzo ya elimu ya Wapiga Kura juu ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura

Tume ya Uchaguzi imepanga kutoa elimu ya wapiga kura kuhusu uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura kwa wanafunzi wa skuli za sekondari 44 na taasisi za elimu ya juu 17 kwa wilaya zote za unguja na pemba.

 

 

JAALA MAKAME HAJI - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada kuhakikisha Elimu ya Wapiga Kura inamfikia kila Mwananchi Mjini na Vijijini ili kuhakikisha kila mwenye sifa anatumia haki yake vizuri ya kujiandikisha na kupiga kura.

Katika kulifikia lengo hilo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa elimu ya Wapiga Kura katika skuli mbali mbali za sekondari pamoja na taasisi za Elimu ya juu za Unguja na Pemba ambazo zimeanza kutolewa kuanzia tarehe 11/04/2019 kwa upande wa Unguja na tarehe 15/04/2019 kwa upande wa Unguja.

Akifungua Muhadhara wa Wanafunzi wa skuli ya biashara ya Chwaka, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jokha Khamis Makame aliwataka vijana ambao hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya maandalizi mapema kwa kutafuta vitambulisho vya mzanzibar mkaazi ili waweze kuandikishwa Daftari hilo siku ikifika.

Mhe. Jokha alisisitiza kwamba, kuwa Mwanafunzi sio kikwazo cha kuandikishwa katika Daftari la kudumu la Wapiga Kura pale ambapo atakuwa ametimiza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura.

Katika muhadhara uliofanyika chuo kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Ndugu. Thabiti Idarous Faina aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuandikishwa na kuhakiki taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura muda ukifika kwani huwezi kupiga kura bila kuandikishwa au kuhakiki taarifa za Mpiga Kura.

Wakiwasilisha mada katika mihadhara mbali mbali iliyofanyika katika skuli mbalimbali za sekondari na taasisi za elimu ya juu maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walisemo Tume hivi sasa imo katika maandalizi ya Uandikishaji ambao utahusisha uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa Taarifa za Wapiga Kura waliomo ndani ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya MWERA Wilaya ya kati wakisikiliza kwa makini mafunzo ya Elimu ya Wapiga Kura yaliyofanyika tarehe 16/04/2019 katika ukumbi wa skuli hiyo (PICHA MAKTABA YA ZEC).

Aidha, Maafisa hao walisisitiza kwamba wakati zoezi la uandikishaji linaendelea shughuli nyengine za uendelezaji wa Daftari kama vile kuhamisha taarifa na kufanya masahihisho ya taarifa hazitofanyika na badala yake kazi hizo zitafanyika katika Ofisi za Wilaya za Uchaguzi mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa. Waombaji watatakiwa waende katika vituo vyao vya asili walivyopiga kura mara ya mwisho kwa uhakiki wa taarifa zao.

Msaidizi Ofisa Uchaguzi wa Wilaya Kaskazini “A” Bibi Miza Pandu Ali akiwasilisha mada katika afunzo ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Uzini.(PICHA NA MAKTABA YA ZEC)

Wapiga Kura waliopoteza shahada zao au kuharibika wote nao watatakiwa kufika vituoni walimojiandikisha na wanatakiwa wachukue vitambulisho vya mzanzibar mkaazi vilivyohakikiwa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaendelea kutoa elimu ya Wapiga Kura kuhusu mwongozo wa uandikishaji na uhakikia wa Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo jumla ya wanafunzi wa Skuli za sekondari 44 na Taasisi za Elimu ya juu 17 Unguja na Pemba wanatarajiwa kufaidika na Elimu hiyo.

Wakufunzi wa mafunzo ya Wajumbe wa Tume za Uchaguzi NEC na ZEC wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji Mkuu mtahafu HAMID MAHMOUD HAMID (hayupo pichani)

 

 

Linki za Haraka


Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii