MAANA YA UCHAGUZI NA MAMBO YA KUFANYA KATIKA MATAYARISHO YA UCHAGUZI

Uchaguzi hasa wa viongozi katika nchi ni utaratibu (mchakato) rasmi unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi kwa njia ya kuwapigia kura kuwachagua watu ambao wanawataka kuwaongoza kwa kipindi maalum. Uchaguzi ni utaratibu wa kawaida wa demokrasia wa kuwapata wawakilishi wa kisiasa ambao umekuwa ukitumika tangu karne ya 17. Kuna aina tatu za msingi za uchaguzi zinazotumiwa kuwapata viongozi kulingana na mfumo unaotumiwa na nchi husika. Aina hizo ni uchaguzi wa Rais, Uchaguzi wa Wawakilishi katika Baraza la Kutunga Sheria na Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa. Vyama vya Siasa kwa upande wao navyo huendesha chaguzi ambazo zinajulikana kwa jina la “Chaguzi wa Msingi” zinazotumika kuwachagua wateuliwa wa vyama katika aina za uchaguzi ambazo zimetajwa hapo juu.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Sheria ya Uchaguzi Na.4, 2018 kifungu cha 3 inauelezea Uchaguzi  kuwa maana yake Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi au Madiwani na inahusiana na Uchaguzi Mdogo na Uchaguzi wa Marejeo. Uchaguzi katika nchi ya Zanzibar unafanywa kwa mujibu wa maelekezo ya Sheria ya Uchaguzi. Kifungu cha 34(1) kinaeleza kuwa “kwa mujibu wa masharti ya Katiba, kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambao utafanyika kila baada ya miaka mitano”.

Kifungu cha (2) cha Sheria hiyo kinaeleza kuwa kinaeleza kuwa Uchaguzi Mkuu chini ya kifungu kidogo cha (1) utajumuisha  uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Pamoja  na maelezo hayo, Sheria inaruhusu kufanyika kwa Uchaguzi Mdogo ambao kwa mujibu wa maelezo ya kifungu cha 40(1) cha Sheria ya Uchaguzi, uchaguzi mdogo utafanyika kutokana na mambo yafuatayo:-

  • Kwa upande wa Rais, utafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu kidogo cha (1) cha kifungu cha 34 cha Katiba;
  • Kwa upande wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, ufanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu kidogo cha (1) cha kifungu cha 71 cha Katiba; na
  • Kwa upande wa Diwani, utafanyika kutokana na kifo, kujiuzulu au sababu nyengine yoyote ambayoitamfanya Diwani kupoteza sifa ya kuwa Diwani.

Kwa kawaida Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hufanya maandalizi ya uchaguzi mdogo mara baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka katika mamlaka  kama vile Baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika na masuala ya Serikali za Mitaa kwa kiti kilicho wazi cha Uwakilishi au Udiwani. 

 

Vile vile, pale ambapo Tume itakuwa haikuridhika kabla ya kutangaza matokeo ya uchaguzi kwamba kulikuwa na kutokufuatwa kwa taratibu , matumizi mabaya au ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi au pale ambapo kura za wagombea waliopata kura za juu imelingana, Tume itasimamisha au kufuta uchaguzi au sehemu yoyote ya uchaguzi na itatangaza siku nyengine ya kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Bofya hapa kwa maelezo zaidi

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii