Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imepongezwa kwa utoaji wa Elimu ya Wapiga Kura kwa Taasisi mbali mbali jambo ambalo linakuza Demokrasia nchini.

Pongezi hizo  zimetolewa na viongozi wa Vyuo Vikuu Tanzania  ambao ni wajumbe wa  Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO)  walipokuwa katika Mkutano Mkuu wa Pili wa Jumuiya hiyo ambapo mada mbali mbali zilijadiliwa, Mkutano ambao umefanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha SUZA kilichopo Tunguu Wilaya ya Kati Unguja, ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Rais wa TAHLISO uliofanyika tarehe 06 Aprili 2024.

Akitoa pongezi zake ndugu.Raifa Abdallah Makame  ambae aliteuliwa katika Mkutano huo kuwa ni Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya TAHLISO mara   baada ya kupatiwa Elimu ya Wapiga Kura alisema  katika Mkutano huo wamejifunza vitu mbali mbali ikiwemo namna ya kupiga kura pasina kuharibika lakini na kujua kanuni mbali mbali zinazomuhusu Mpiga Kura hali ambayo utaufanya Uchaguzi wa TAHLISO uwe wa huru na haki kwani kila Mpiga Kura sasa anajua haki yake katika Uchaguzi huo.

Sambamba na hilo aliwapongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa kuwapatia muamko huo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri  kwa vijana wengine.

Nae Khamis Abam Dilo ambae ni mshiriki wa Mkutano huo lakini pia ni Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya TAHLISO alishukuru kuwa moja ya washiriki waliopatiwa Elimu ya Wapiga Kura kwani mafunzo hayo yamemuwezesha kujua mipaka yake katika zoezi la Uchaguzi,

Aliwaasa Wajumbe wa Mkutano huo Kupiga Kura kwa salama na amani kwani kuna maisha baada ya Uchaguzi.

Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo  ndugu.Mohammed Idrissa Haji ambae ni Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Wapiga Kura alisema lengo la kuwapatia elimu hiyo ni kuwawezesha kuwa na uelewa sahihi kuhusu zoezi la Upigaji wa Kura na kujua  Kanuni na Sheria zinazosimamia Uchaguzi ili kupunguza idadi ya Kura kuharibika katika Chaguzi mbali mbali ikiwemo zinaezoendeshwa na Taasisi za Elimu.

Aliwakumbusha Wajumbe wa Mkutano huo kuyazingatia Mafunzo kwani tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani 2025 ambapo wananchi watapata nafasi ya kuchagua viongozi mbali mbali hivyo ni vyema kuizingatia elimu hiyo.

Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha SUZA ulijumuisha Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO ambao ni Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na Maspika wa Serikali za Wanafunzi nchini.

Katika Mkutano huu uliolenga kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za Wanafunzi, Wadau na Wageni mbalimbali maalumu wameshiriki ikiwemo Wadau kutoka NHIF,NACTVET, HESLB, CRDB, NMB,Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Wadau wa Bodi ya Mikopo kutoka Tanzania Bara na visiwani Zanzibar.

 

 

Viongozi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Wageni mbali mbali wakiwa kwenye futari iliyoandaliwa na Tume hiyo katika Afisi Kuu zilizopo Maisara,Mjini Unguja tarehe 30 Machi 2024.

Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) imeendesha mafunzo ya siku moja ya kuwajenga uwezo na uelewa juu ya utoaji huduma wa Mfuko huo visiwani Zanzibar.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika ukumbi wa Afisi ya Tume ya Uchaguzi ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ iliyopo Mwera nje kidogo ya jiji la Zanzibar  lengo likiwa ni kuwaandaa wadau muhimu katika  matumizi ya Mfuko huo nchini.

Akifungua mafunzo hayo Afisa Masoko na Uhusiano kutoka Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF)  Asha Kassim Mbiwi  alisema Mfuko huo umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba 1 ya mwaka 2023 ambayo ni   Sheria ya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar,Sheria  ambayo ina umuhimu mkubwa nchini kwani inalenga katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote za uhakika na endelevu kwa wananchi na wakaazi wote wa Zanzibar na kuhakikisha upatikanaji wa rasimali fedha za kutosha na endelevu za kugharamia huduma za afya kwa wote hatua ambayo itaweza  kuweka mazingira bora ya kukuza na kustawisha huduma za Afya nchini.

Akizungumzia baadhi ya majukumu ya Mfuko huo alisema unajikita katika kulipia huduma za Afya kwa  wanachama na wategemezi wao,kukusanya, kuhifadhi na kusimamia michango ya wanachama pamoja na fedha nyengine zitakazolipwa na kulinda maslahi ya wanachama.

 Aliwakumbusha washiriki kuyatumia vyema mafunzo hayo ili kujijengea uelewa wakutosha  na uelewa sahihi wa Mfuko huo kwani wadau mbali mbali wamekuwa na maswali mengi juu ya Mfuko huo.

“kupitia mafunzo haya mtaweza kuuliza maswali ya kina pamoja na kutoa maoni yenu muhimu kuhusu huduma hii ili tuweze kuyazingatia na kuyatekeleza kwa maslahi ya wananchi wetu hapa Zanzibar  hasa nyinyi wafanyakazi wa Serikali ambao ni miongoni mwa makundi ya kwanza kufikiwa katika elimu hii ambayo ilianza kwa ngazi za juu za viongozi wa juu wa kila Taasisi za Serikali ya Zanzibar’’ alisema.

Aidha,  alisema wataendelea na program za kutoa elimu kwa Taasisi za Serikali hadi pale watakapokamilisha kutoa mafunzo kwa Taasisi zote za Serikali na zoezi kama hilo linafanyika Unguja na Pemba na zoezi kama hili litafanyika pia kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.

Akitoa ufafanuzi juu ya maswali mbali mbali yaliyoulizwa katika mafunzo hayo Bi.Asha  alisema Mfuko huo bado haujawafikia Wazanzibar wote na umeanza kwa Wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini malengo ni kuwafikia Wazanzibar wote na Mfuko huo unaamini kuwa taarifa muhimu kuhusu huduma hiyo mpya zitawafikia walengwa wote kote nchini,

Nae Afisa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Bi Mwanamkuu Gharib Mgeni Alisema mafunzo hayo yamewapa faraja wafanyakazi wa Tume kwani wameelewa jinsi Mfuko unavyofanya kazi na walengwa wa Mfuko huo,na mafunzo hayo yamewanufaisha na kujua azma ya Serikali na muelekeo wake,amewaasa wafanyakazi kutoiacha fursa hiyo muhimu kwani huwezi kufanya kazi ukiwa huna afya bora.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Wafanyakazi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mkuu wa kurugenzi ya Huduma za Sheria ndugu.Maulid   aliwashukuru na kuwapongeza kwa kuwapatia mafunzo hayo juu ya Mfuko huo.

 

 

Maafisa Wilaya wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) wameshiriki katika uangalizi wa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani kwa upande wa Tanzania Bara ambapo wagombea 127 kutoka vyama 18 vya siasa wameshiriki katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata 22 za Tanzania Bara, Uchaguzi uliofanyika tarehe 20 Machi, 2024.

Akitoa pongezi zake kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na wananchi waliojitokeza katika Uchaguzi huo Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi ‘B’ Khadija M. Ali, wakati wa kutembelea
Vituo vya Kupigia Kura Kata ya Kimbiji Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Mkoa wa Dar-es-Salaam alisema wadau wote wakiwemo wapiga kura na wananchi katika kata hiyo wamefanya Uchaguzi kwa utulivu mkubwa na mwitikio wa wananchi katika kata hiyo umekuwa wakuridhisha.

Sambamba na Hilo ameipongeza Tume ya Uchaguzi ya Taifa NEC kwa kuwapa mualiko huo kwani unaendeleza mashirikiano mazuri na mema baina ya Tume hizo mbili katika masuala ya kitaifa yanayohusiana na Uchaguzi.

Nae Issa Juma Hamad Msaidizi Afisa Uchaguzi Wilaya ya Micheweni ambae alitembelea vituo vya kupigia Kura katika kata ya Msangani Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoa wa Pwani pamoja na Mahmoud Ahmada kutoka Wilaya ya Mkoani aliwashauri wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi huo wa Madiwani.

“wito wangu kwa Wapiga Kura wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kwa ajili ya kuchagua madiwani wetu ambayo kila”

Aidha, aliwaomba Wapiga Kura kutekeleza jukumu hilo kwa utulivu na amani kwani kuna maisha baada ya Uchaguzi huo Mdogo.

Katika uangalizi huo Maafisa 4 wameshiriki katika Uchaguzi huo ambao ni Msaidizi Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Kati Said H. Vuai na Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi ‘B’ Khadija M. Ali, Issa J. Hamad kutoka Wilaya ya Micheweni na Mahmoud A. Mbwana kutoka Wilaya ya Mkoani Pemba,

ZEC na NEC zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali ya Kiuchaguzi kwa mujibu wa Kifungu cha 119 (14) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

 

 

Wanasiasa watakiwa kubadilika na kuwa wakweli  ili kuepuka kuopotosha Umma

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji George J. Kazi amewataka Wanasiasa kubadilika na kuwa wakweli wanapoeleza  shughuli zinazofanywa na Tume hiyo ili kuepusha siasa za Uchochezi na hatimae kuibakisha nchi ikiwa salama.

Alisema kuendelea kuwapa habari wananchi zisizo na ukweli ni sawa na upotoshaji kwani mambo yote yanayoendeswa na Tume hayafichwi yako wazi na kila mmoja anaona na wadau mbali mbali wamekuwa wakishirikishwa katika kazi za ZEC ikiwemo Uandikishaji Wapiga Kura.

Jaji Kazi, alieleza hayo huko katika ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake Chake Pemba katika Mkutano wa Tathmini ya zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya kwenye Daftari la kudumu  lililoendeshwa na Tume hiyo kwa Mikoa yote ya Zanzibar kuanzia tarehe  2 Disemba  2023 hadi tarehe 15 Januari 2024.

Alisema kuwa wakati wa Zoezi la Uandikishaji likiendeshwa viongozi wote wa Tume hiyo walikuwa wakifuatilia na kulikuwa na mashirikiano makubwa baina ya watendaji na Mawakala wa Vyama vya Siasa ,hivyo dosari yoyote ilikuwa inajitokeza ilikuwa inapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake hiyo.

“ Watendaji wote wa Tume hii walikuwa hawakai Ofisini kuanzia mwanzo wa zoezi mpaka mwisho wa zoezi hivyo changamoto zote ambazo zilikuwa zinajitokeza katika zoezi hilo zilipatiwa ufumbuzi wa pamoja na nichukuwe fursa hii kuwapongeza wadau wote kwa ushirikiano wenu mulioipatia Tume yetu”, alisema.

 

 

Akizungumzia kumalizika kwa zoezi hilo Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa zoezi lilikwenda vyema kwa Amani na utulivu.

Alisema katika zoezi hilo jumla ya Wapiga Kura Wapya  57,883wameandikishwa wakiwemo Wanawake 31,440 na Wanaume 26,443 sawa asilimia 35.6 ya walioandikishwa ingawaje matarajio ni kuandikisha Wapiga Kura Wapya 162,606, lakini pamoja na zoezi hilo kumalizika kazi inayofuata ni kuweka wazi Daftari kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 1 hadi 7 Machi 2024.

Aliwataka Wadau wa Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kuwahamasisha Vijana waliomba kuandikishwa kwenda vituoni kuangalia taarifa zao kwani kufika kwao vituoni kuona taarifa zao kutawarahisishia nafasi ya kuwemo katika Daftari na kuwa Wapiga Kura.

“ Tume inawaomba Wananchi  muendelee kudumisha Amani na utulivu ndani ya nchi yetu na kutoa ushirikiano mzuri kwa shughuli zinazoendeshwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar katika mzunguko wote wa Uchaguzi”, alisema.

Akitoa Tathmini ya Wapiga Kura wapya awamu ya kwanza Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar , Thabit Idarous Faina alisema kuwa kifungu cha 19 ( 1) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2018 kinaelekeza afisa Uandikishaji baada ya kukamilika kwa Uandikishaji Wapiga Kura kwa kufuata miongozo ya Tume ataweka wazi orodha ya waombaji wapya katika kila kituo cha Uandikishaji kwa muda wa siku 7.

Alifahamisha sambamba na hilo pia kifungu cha 19 (2) kinaeleza kuwa Mpiga Kura yoyote au muombaji anaweza kuchunguza orodha ya Wapiga kura  iliowekwa wazi kwa madhumuni ya kuthibitisha kuwa yumo, kuangalia usahihi wa taarifa zake au kuweka pingamizi taarifa za muombaji mwengine asiekuwa na sifa katika orodha hiyo.

Alieleza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa mujibu wa mpango kazi wake itaendesha zoezi kama hilo kwa awamu ya pili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2025.

“ Niwahakikishie wadau Uchaguzi kuwa shuguli zote zinazofanywa na Tume hii zinakwenda kwa mujibu wa Sheria na sio kwa matakwa ya watu wengine “, alisema

Alifahamisha kuwa wakati wa zoezi hilo wadau mbali mbali walishirikishwa na Tume kuanzia ngazi ya mwanzo hadi ya mwisho kwa mujibu wa nafasi zao wakiwemo  Vyama vya Siasa, vikosi vya Ulinzi na Usalama, asasi za kijamii Vyombo vya habari , makundi maalumu nakadhalika.

Mkurugenzi huyo alisema katika kufanikisha zoezi hilo kwa mujibu wa Sheria namba 4 ya mwaka 2018 , kifungu cha 14 (1) Vyama vya Siasa viliruhusiwa kuweka Mawakala wao katika vituo vyote vya Uandikishaji ili kuangalia mwenendo wa Uandikishaji ambapo jumla ya Vyama 14 viliweka Mawakala wao.

Alieleza vyama 5 vya siasa havikuweka Mawakala wao katika zoezi hilo kwa sababu zao mbali mbali, aidha asasi za kiraia 10 zilishiriki zoezi hilo .

Aliwapongeza wadau wote wa Uchaguzi kwa ushiriki wao katika kufanikisha zoezi hilo na kuwataka waendelee kudumisha Amani na utulivu kwani ndio uliowezesha kufanyika kwa kazi hiyo muhimu ya Kidemokrasia.

Nae Mkurugenzi wa Huduma za Uchaguzi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndugu Khamis Issa Khamis alisema mpaka kufikia tarehe 15 Febuari mwaka 2024 jumla ya wapigakura 323 wameshawasilisha maombi ya kuhamisha taarifa zao kutoka eneo moja kwenda jengine la Uchaguzi.

Alieleza kuwa uhamisho wa taarifa za Wapiga kura ni endelevu  na kazi ya kupokea taarifa za wanaoomba kuhamisha inaendelea kufanyika katika Afisi za Uchaguzi za Wilaya kila siku kwa saa za kazi.

Hata hivyo Tume inawasisitiza wananchi kudumisha Amani na Utulivu wakati wa zoezi la kuangalia taarifa zao sambamba na kutowa ushirikiano mkubwa ili zoezi liende vizuri.

 

           

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii