ABOUJA - NIGERIA

Jaala Makame Haji- ZEC

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe. Jaji Mkuu (Mst) Hamid Mahmoud Hamid ameushauri mtandao wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Magharibi mwa Afrika kulipa umuhimu suala la uwakilishi wa makundi maalum katika mamlaka za kutunga Sheria.

Mwenyekiti Hamid Mahmoud ameushauri mtandao huo wakati alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Tume za Uchaguzi za nchi za kusini mwa Afrika (ECF-SADC) katika mkutano wa sita ulioandaliwa na mtandao wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Magharib mwa Afrika (ECONEC) nchini Nigeria.

Mhe. Hamid amesisitiza kuwa, ushiriki wa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu katika hatua zote za michakato ya Kiuchaguzi ni hatua nzuri ambayo inaonesha ukomavu wa kisiasa na utekelezaji wa misingi ya kidemokrasia katika nchi za Magharib mwa Afrika.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji Mkuu (Mst) Hamid Mahmoud akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Tume za Uchaguzi za nchi za kusini mwa Afrika (ECF-SADC) katika mkutano wa sita ulioandaliwa na mtandao wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Magharib mwa Afrika (ECONEC) nchini Nigeria.

 Aidha, Mwenyekiti Hamid aliendelea kusema kuwa, mtandao wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Magharib mwa Afrika umeamuwa kufanya kongamano hilo ili kujadili namna ya kukuza ushirikishwaji katika michakato ya kiuchagzui kwani uchaguzi ni mchakato mkubwa ambao unahitaji umakini na maamuzi ya pamoja  katika  uendeshaji wake.

Sambamba na hayo, alifafanua kuwa, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni miongoni mwa Tume za  nchi za kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinathamini maoni inayotolewa na Wadau wa Uchaguzi wakiwemo Waangalizi wa Uchaguzi pamoja na Wanasiasa ambapo maoni hayo  yamekuwa yakitumika kuimarisha Sheria za Uchaguzi za miongoni mwa Nchi za SADC

Mkutano mkuu wa sita wa mtandao wa Tume za Uchaguzi za Nchi za Magharibi mwa Afrika ECONEC ambao unafanyika nchini Nigeria umewasirikisha wadau wa siasa katika masula ya kiuchaguzi wakiwemo, viongozi wa Tume za Uchaguzi, mamlaka za kutunga Sheria, wataalamu wa masuala ya jinsia, wanaharakati wa makundi ya vijana na  watu wenye ulemavu    

Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imesema kuwa itahakikisha inafuata misingi ya uwazi na kuwashirikisha wadau wa Uchaguzi katika kuendesha kura ya mapema ambayo itafanyika katika uchaguzi mkuu ujao kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 1 ya mwaka 2018.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji mkuu (Mstaafu) Hamid Mahmoud Hamid alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Afisi ya Tume hiyo wakati alipofanya mazungumzo na viongozi wa mtandao wa uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TASEO).

Katika mazungumzo hayo ambayo yanalenga kukuza ushirikiano wa ZEC na wadau wa uchaguzi mwenyekiti Hamid aliwaeleza viongozi wa mtandao huo wa uangalizi wa Uchaguzi kwamba, Tume ya Uchaguzi itaendelea kufanya  ziara za kimasomo katika nchi ambazo zinafanya kura ya mapema ili kupata uzoefu wa nchi hizo.

 

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Jaji Mkuu (Mst) Hamid Mahmoud Hamid (kulia) akifafanua jambo kwenye kikao na Uongozi wa mtandao wa waangalizi wa Uchaguzi Tanzania (kushoto makamo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Mabrouk Jabu Makame) (Picha na Tume ya Uchaguzi).

Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabiti Idarous Faina alisema, kwa kuwa Zanizbar ndio mara ya kwanza kufanya kura ya mapema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itatumia kila njia kufikisha elimu ya wapiga kura ili kuondosha mikanganyiko ambayo inaweza kujitokeza wakati wa kuendesha kura hiyo ya mapema

Mkurugenzi Faina aliendelea kusema kwamba, Tume haitosita kuvitumia vyombo vya habari katika kutoa Elimu na kutoa taarifa kwa Wananchi katika kila hatua ya Uchaguzi ili kuwa na uelewa sahihi

Akizungumzia kuhusu Kura ya Mapema Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Khamis Issa Khamis alisema, utaratibu wa kufanyika kura ya Mapema umezungumzwa katika Sheria ya Uchaguzi Nam. 1 Ya mwaka 2018 kwa lengo la kuwapa fursa baadhi ya wananchi ambao hukosa kupiga kura kutokana na majukumu yao siku ya kupiga kura.

Ndugu Khamis, aliwaasa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuacha kupotosha wananchi kuhusu utaratibu wa kufanyika kura ya mapema na badala yake kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi hao ili kuepuka uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya Mtandao wa Uangalizi wa uchaguzi Tanzania  mkurugenzi mtendaji wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC)  Harusi Miraji Mpatani aliishukuru na kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa jitihada wanazozichukua kwa kuwashirikisha Wadau wa Uchaguzi katika kila hatua ya Uchaguzi.

 

 

JAALA MAKAME HAJI- ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imewaomba Wapiga Kura waliomo ndani ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya kuhakiki taarifa zao muda ukifika ambapo kazi hiyo ya uhakiki itafanyika sambamba na kazi ya kuandikisha Wapiga Kura wapya katika daftari hilo kwa mujibu wa ratiba itakayotolewa na tume.

Akizungumza katika semina ya wanafunzi wa skuli za sekondari za wilaya ya Magahrib “A” Afisa Uchaguzi wa Wilaya hiyo ndugu. Ali Rashid Suluhu alisema wapiga kura wote watapaswa kuhakiki taarifa zao za kitambulisho cha mzanzibar mkaazi ambacho kitawawezesha kuhakiki taarifa zao katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwani bila kuhakiki taarifa huwezi kupiga kura kwa Uchaguzi ujao.

Akizungumzia kuhusu uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya ndugu Suluhu aliwata wazazi na walezi kuwahamasisha vijana ambao wamefikia umri wa miaka kumi nane ambao hawana vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi kufanya jitihada za makusudi kupata vitambulisho hivyo ili nawao waweze kuandikishwa kuwa Wapiga Kura muda ukifika.

Naye msaidizi Afisa uchaguzi Wilaya ya Kaskazini “A” Bi Miza Pandu Ali alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itaweka wazi majina ya wapiga kura katika vituo vyote vya kujiandikisha baada ya kumaliza kazi ya uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Bi Miza Pandu alifahamisha kwamba, lengo la kuweka wazi majina ya wapiga kura ni kuwapa fursa wapiga kura kujiridhisha kuhusu usahihi wa taarifa zao na kuweka pingamizi kwa wapiga kura ambao hawana sifa za kuandikishwa katika eneo husika.

Bi Miza aliongeza kusema kwamba, wakati wa zoezi la uandikishaji Tume haitofanya shuhuli za uendelezaji wa Daftari kwa wapiga Kura wanaoomba kubadilisha na kusahihisha taarifa zao pamoja na Wapiga Kura waliopoteza shahada zao na badala yake shuhuli hizo zitafanyika katika ofisi za Uchaguzi za Wilaya mara baada ya kukamilika kwa kazi ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa.

Kwa nyakati tofauti wanafunzi wa skuli za sekondari za Wilaya ya Magharib “A” wameiomba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuendelea kutoa elimu ya Wapiga Kura ili kila mwananchi aweze kutumia haki yake ya kupiga kura muda ukifika.

Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Kaskazini A Ndg. BAKAR BURHANI SULEIMAN akizungumza na wanafunzi wa skuli ya sekondari ya Bububu katika mafunzo ya elimu ya Wapiga Kura juu ya Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura

Tume ya Uchaguzi imepanga kutoa elimu ya wapiga kura kuhusu uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura kwa wanafunzi wa skuli za sekondari 44 na taasisi za elimu ya juu 17 kwa wilaya zote za unguja na pemba.

 

 

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inaendelea kutoa Elimu ya Wapiga Kura kuhusu uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura waliomo katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwa wanafunzi wa skuli zote za Sekondari za Unguja na Pemba.

Akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharib “A” ndugu. ALI RASHID SULUH alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa Elimu ya Wapiga Kura kwa wanafunzi wa skuli za Sekondari ikiwa ni muendelezo wa kazi za maandalizi ya uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Afisa huyo, aliwataka wanafunzi wa Skuli za Sekondari ambao bado hawajaandikishwa katika Daftari la kudumu la wapiga kura kufanya maandalizi ya mapema kwa kutafuta kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ili waweze kuandikishwa katika Daftari hilo siku ikifika.

Wakati huo huo, Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharib “B” KHAMIS MUSSA KHAMIS aliongeza kwa kusema kuwa wakati wa Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam.4 ya 2018 kifungu cha 12(1) Tume, itaendelea kutumia taarifa za kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ambacho kimeboreshwa taarifa zake, hivyo kila Mwananchi anatakiwa afanye maandalizi ya mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa kuomba kuandikishwa au kuhakiki taarifa. “ mwananchi atakayeenda kituoni kuomba kuandikisha au kuhakiki taarifa zake atalazimika kuchukua kitambulisho cha mzanzibar mkaazi kilichohakikiwa ”.

Aidha, Afisa Khamis Mussa alisisitiza kuwa, kila mwananchi anayo haki ya kupiga kura lakini hatoweza kutumia haki hiyo katika Uchaguzi ujao ikiwa haku andikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au kuhakiki taarifa zake.

Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge wakifuatilia kwa makini maelezo ya Elimu ya Wapiga Kura kuhusu uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura tarehe 9/07/2019 (picha Maktaba ya ZEC)

Naye kaimu Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge Ndugu Kassim Mohammed Juma aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa jitihada zao za kuhakikisha kila Mwananchi aweze kutumia haki yake ya Kidemokrasia na kuiomba Tume hiyo kuhakikisha inawafikia wanafunzi wote walioko ng’ambo ya Mji ili nawao wapate elimu hiyo.

Hata hivyo, Mwalim Kassim aliahidi kwamba atakuwa mstari wa mwanzo kuhakikisha anaitumia kwa vitendo elimu hiyo na kuwa balozi mzuri wa kuifikisha kwa walimu, wanafunzi na wananchi kwa jumla.

Mwalim wa Skuli hiyo TATU KHAMIS MOHAMMED alisema utaratibu unaofanywa na ZEC utawafanya wanafunzi wa skuli za Sekondari kutumia vyema haki yao ya kidemokrasia kwa kujiandikisha na kupiga kura kwani hapo awali walikuwa wanafanya kimazoea bila ya kuwa na elimu yeyote .

Kwa nyakati mbali mbali Wanafunzi waliopatiwa Elimu ya Wapiga Kura waliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuiomba kuongeza jitihada katika kufikisha Elimu ya Wapiga Kura kwa Wanzibar wote.

JAALA MAKAME HAJI - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada kuhakikisha Elimu ya Wapiga Kura inamfikia kila Mwananchi Mjini na Vijijini ili kuhakikisha kila mwenye sifa anatumia haki yake vizuri ya kujiandikisha na kupiga kura.

Katika kulifikia lengo hilo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa elimu ya Wapiga Kura katika skuli mbali mbali za sekondari pamoja na taasisi za Elimu ya juu za Unguja na Pemba ambazo zimeanza kutolewa kuanzia tarehe 11/04/2019 kwa upande wa Unguja na tarehe 15/04/2019 kwa upande wa Unguja.

Akifungua Muhadhara wa Wanafunzi wa skuli ya biashara ya Chwaka, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jokha Khamis Makame aliwataka vijana ambao hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya maandalizi mapema kwa kutafuta vitambulisho vya mzanzibar mkaazi ili waweze kuandikishwa Daftari hilo siku ikifika.

Mhe. Jokha alisisitiza kwamba, kuwa Mwanafunzi sio kikwazo cha kuandikishwa katika Daftari la kudumu la Wapiga Kura pale ambapo atakuwa ametimiza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura.

Katika muhadhara uliofanyika chuo kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Ndugu. Thabiti Idarous Faina aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuandikishwa na kuhakiki taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura muda ukifika kwani huwezi kupiga kura bila kuandikishwa au kuhakiki taarifa za Mpiga Kura.

Wakiwasilisha mada katika mihadhara mbali mbali iliyofanyika katika skuli mbalimbali za sekondari na taasisi za elimu ya juu maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walisemo Tume hivi sasa imo katika maandalizi ya Uandikishaji ambao utahusisha uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa Taarifa za Wapiga Kura waliomo ndani ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya MWERA Wilaya ya kati wakisikiliza kwa makini mafunzo ya Elimu ya Wapiga Kura yaliyofanyika tarehe 16/04/2019 katika ukumbi wa skuli hiyo (PICHA MAKTABA YA ZEC).

Aidha, Maafisa hao walisisitiza kwamba wakati zoezi la uandikishaji linaendelea shughuli nyengine za uendelezaji wa Daftari kama vile kuhamisha taarifa na kufanya masahihisho ya taarifa hazitofanyika na badala yake kazi hizo zitafanyika katika Ofisi za Wilaya za Uchaguzi mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa. Waombaji watatakiwa waende katika vituo vyao vya asili walivyopiga kura mara ya mwisho kwa uhakiki wa taarifa zao.

Msaidizi Ofisa Uchaguzi wa Wilaya Kaskazini “A” Bibi Miza Pandu Ali akiwasilisha mada katika afunzo ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Uzini.(PICHA NA MAKTABA YA ZEC)

Wapiga Kura waliopoteza shahada zao au kuharibika wote nao watatakiwa kufika vituoni walimojiandikisha na wanatakiwa wachukue vitambulisho vya mzanzibar mkaazi vilivyohakikiwa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaendelea kutoa elimu ya Wapiga Kura kuhusu mwongozo wa uandikishaji na uhakikia wa Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo jumla ya wanafunzi wa Skuli za sekondari 44 na Taasisi za Elimu ya juu 17 Unguja na Pemba wanatarajiwa kufaidika na Elimu hiyo.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii