Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inaendelea kutoa Elimu ya Wapiga Kura kuhusu uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga kura waliomo katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwa wanafunzi wa skuli zote za Sekondari za Unguja na Pemba.

Akizungumza na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharib “A” ndugu. ALI RASHID SULUH alisema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa Elimu ya Wapiga Kura kwa wanafunzi wa skuli za Sekondari ikiwa ni muendelezo wa kazi za maandalizi ya uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa taarifa za wapiga kura waliomo katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Afisa huyo, aliwataka wanafunzi wa Skuli za Sekondari ambao bado hawajaandikishwa katika Daftari la kudumu la wapiga kura kufanya maandalizi ya mapema kwa kutafuta kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ili waweze kuandikishwa katika Daftari hilo siku ikifika.

Wakati huo huo, Afisa Uchaguzi Wilaya ya Magharib “B” KHAMIS MUSSA KHAMIS aliongeza kwa kusema kuwa wakati wa Uandikishaji na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam.4 ya 2018 kifungu cha 12(1) Tume, itaendelea kutumia taarifa za kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi ambacho kimeboreshwa taarifa zake, hivyo kila Mwananchi anatakiwa afanye maandalizi ya mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa kuomba kuandikishwa au kuhakiki taarifa. “ mwananchi atakayeenda kituoni kuomba kuandikisha au kuhakiki taarifa zake atalazimika kuchukua kitambulisho cha mzanzibar mkaazi kilichohakikiwa ”.

Aidha, Afisa Khamis Mussa alisisitiza kuwa, kila mwananchi anayo haki ya kupiga kura lakini hatoweza kutumia haki hiyo katika Uchaguzi ujao ikiwa haku andikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura au kuhakiki taarifa zake.

Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge wakifuatilia kwa makini maelezo ya Elimu ya Wapiga Kura kuhusu uandikishaji na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura tarehe 9/07/2019 (picha Maktaba ya ZEC)

Naye kaimu Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Mwenge Ndugu Kassim Mohammed Juma aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa jitihada zao za kuhakikisha kila Mwananchi aweze kutumia haki yake ya Kidemokrasia na kuiomba Tume hiyo kuhakikisha inawafikia wanafunzi wote walioko ng’ambo ya Mji ili nawao wapate elimu hiyo.

Hata hivyo, Mwalim Kassim aliahidi kwamba atakuwa mstari wa mwanzo kuhakikisha anaitumia kwa vitendo elimu hiyo na kuwa balozi mzuri wa kuifikisha kwa walimu, wanafunzi na wananchi kwa jumla.

Mwalim wa Skuli hiyo TATU KHAMIS MOHAMMED alisema utaratibu unaofanywa na ZEC utawafanya wanafunzi wa skuli za Sekondari kutumia vyema haki yao ya kidemokrasia kwa kujiandikisha na kupiga kura kwani hapo awali walikuwa wanafanya kimazoea bila ya kuwa na elimu yeyote .

Kwa nyakati mbali mbali Wanafunzi waliopatiwa Elimu ya Wapiga Kura waliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na kuiomba kuongeza jitihada katika kufikisha Elimu ya Wapiga Kura kwa Wanzibar wote.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii