Jaala Makame Haji - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imesema kuwa itahakikisha inafuata misingi ya uwazi na kuwashirikisha wadau wa Uchaguzi katika kuendesha kura ya mapema ambayo itafanyika katika uchaguzi mkuu ujao kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 1 ya mwaka 2018.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jaji mkuu (Mstaafu) Hamid Mahmoud Hamid alitoa kauli hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Afisi ya Tume hiyo wakati alipofanya mazungumzo na viongozi wa mtandao wa uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TASEO).

Katika mazungumzo hayo ambayo yanalenga kukuza ushirikiano wa ZEC na wadau wa uchaguzi mwenyekiti Hamid aliwaeleza viongozi wa mtandao huo wa uangalizi wa Uchaguzi kwamba, Tume ya Uchaguzi itaendelea kufanya  ziara za kimasomo katika nchi ambazo zinafanya kura ya mapema ili kupata uzoefu wa nchi hizo.

 

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Jaji Mkuu (Mst) Hamid Mahmoud Hamid (kulia) akifafanua jambo kwenye kikao na Uongozi wa mtandao wa waangalizi wa Uchaguzi Tanzania (kushoto makamo mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Mabrouk Jabu Makame) (Picha na Tume ya Uchaguzi).

Mkurugenzi wa Uchaguzi Thabiti Idarous Faina alisema, kwa kuwa Zanizbar ndio mara ya kwanza kufanya kura ya mapema, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar itatumia kila njia kufikisha elimu ya wapiga kura ili kuondosha mikanganyiko ambayo inaweza kujitokeza wakati wa kuendesha kura hiyo ya mapema

Mkurugenzi Faina aliendelea kusema kwamba, Tume haitosita kuvitumia vyombo vya habari katika kutoa Elimu na kutoa taarifa kwa Wananchi katika kila hatua ya Uchaguzi ili kuwa na uelewa sahihi

Akizungumzia kuhusu Kura ya Mapema Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Khamis Issa Khamis alisema, utaratibu wa kufanyika kura ya Mapema umezungumzwa katika Sheria ya Uchaguzi Nam. 1 Ya mwaka 2018 kwa lengo la kuwapa fursa baadhi ya wananchi ambao hukosa kupiga kura kutokana na majukumu yao siku ya kupiga kura.

Ndugu Khamis, aliwaasa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuacha kupotosha wananchi kuhusu utaratibu wa kufanyika kura ya mapema na badala yake kutumia nafasi zao kuwaelimisha wananchi hao ili kuepuka uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya Mtandao wa Uangalizi wa uchaguzi Tanzania  mkurugenzi mtendaji wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC)  Harusi Miraji Mpatani aliishukuru na kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa jitihada wanazozichukua kwa kuwashirikisha Wadau wa Uchaguzi katika kila hatua ya Uchaguzi.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii