JAALA MAKAME HAJI - ZEC

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada kuhakikisha Elimu ya Wapiga Kura inamfikia kila Mwananchi Mjini na Vijijini ili kuhakikisha kila mwenye sifa anatumia haki yake vizuri ya kujiandikisha na kupiga kura.

Katika kulifikia lengo hilo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inatoa elimu ya Wapiga Kura katika skuli mbali mbali za sekondari pamoja na taasisi za Elimu ya juu za Unguja na Pemba ambazo zimeanza kutolewa kuanzia tarehe 11/04/2019 kwa upande wa Unguja na tarehe 15/04/2019 kwa upande wa Unguja.

Akifungua Muhadhara wa Wanafunzi wa skuli ya biashara ya Chwaka, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe. Jokha Khamis Makame aliwataka vijana ambao hawajaandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kufanya maandalizi mapema kwa kutafuta vitambulisho vya mzanzibar mkaazi ili waweze kuandikishwa Daftari hilo siku ikifika.

Mhe. Jokha alisisitiza kwamba, kuwa Mwanafunzi sio kikwazo cha kuandikishwa katika Daftari la kudumu la Wapiga Kura pale ambapo atakuwa ametimiza sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura.

Katika muhadhara uliofanyika chuo kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Ndugu. Thabiti Idarous Faina aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuandikishwa na kuhakiki taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura muda ukifika kwani huwezi kupiga kura bila kuandikishwa au kuhakiki taarifa za Mpiga Kura.

Wakiwasilisha mada katika mihadhara mbali mbali iliyofanyika katika skuli mbalimbali za sekondari na taasisi za elimu ya juu maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar walisemo Tume hivi sasa imo katika maandalizi ya Uandikishaji ambao utahusisha uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa Taarifa za Wapiga Kura waliomo ndani ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya MWERA Wilaya ya kati wakisikiliza kwa makini mafunzo ya Elimu ya Wapiga Kura yaliyofanyika tarehe 16/04/2019 katika ukumbi wa skuli hiyo (PICHA MAKTABA YA ZEC).

Aidha, Maafisa hao walisisitiza kwamba wakati zoezi la uandikishaji linaendelea shughuli nyengine za uendelezaji wa Daftari kama vile kuhamisha taarifa na kufanya masahihisho ya taarifa hazitofanyika na badala yake kazi hizo zitafanyika katika Ofisi za Wilaya za Uchaguzi mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uandikishaji na uhakiki wa taarifa. Waombaji watatakiwa waende katika vituo vyao vya asili walivyopiga kura mara ya mwisho kwa uhakiki wa taarifa zao.

Msaidizi Ofisa Uchaguzi wa Wilaya Kaskazini “A” Bibi Miza Pandu Ali akiwasilisha mada katika afunzo ya Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Uzini.(PICHA NA MAKTABA YA ZEC)

Wapiga Kura waliopoteza shahada zao au kuharibika wote nao watatakiwa kufika vituoni walimojiandikisha na wanatakiwa wachukue vitambulisho vya mzanzibar mkaazi vilivyohakikiwa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaendelea kutoa elimu ya Wapiga Kura kuhusu mwongozo wa uandikishaji na uhakikia wa Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo jumla ya wanafunzi wa Skuli za sekondari 44 na Taasisi za Elimu ya juu 17 Unguja na Pemba wanatarajiwa kufaidika na Elimu hiyo.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii