Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud amepongeza uteuzi wa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)  na kuongeza kuwa Wananchi wana imani na Tume hiyo.

Mhe.Ayoub ameyasema hayo jana,tarehe 7 Septemba,2023 wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji George Joseph Kazi na Wajumbe sita wa Tume hiyo pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Ndugu.Thabit Idarous Faina na baadhi ya Wakuu wa Kurugenzi na Divisheni,walipotembelea Afisi za Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud katika Afisi zake Mkokotoni, Kaskazini Unguja, wakati wa ziara ya Mwenyekiti huyo katika Afisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mkoani humo.

Amesema Uteuzi wa Tume hiyo umewapa heshima kubwa si tu kwao binafsi bali kwa nchi nzima na imani waliyopewa na Rais ni imani hiyo hiyo watakayokuwa nayo wananchi,hivyo  wanamatumaini kuwa watavuka Salama Katika Uchaguzi Mkuu wa Mkuu wa 2025 na utakuwa ni Uchaguzi wa salama na amani ulio huru na haki kwani nchi yetu imekuwa kidemokrasia na Tume hiyo pia imekuwa kidemokrasia, ameongeza kuwa Tume hiyo itakubaliwa na Wananchi na matokeo ya Uchaguzi Tume hiyo itakayoyatoa yatakubaliwa na wananchi.

Amesema,kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja watatoa kila mashirikiano ili kuhakikisha kazi ya Tume hiyo inakuwa nyepesi na watahakikisha wanawahamasisha na kuwaelimisha wananchi kufuata Sheria za Uchaguzi pale nyakati zitakakapofika bila ya kuvutana na anaamini Wananchi waliowengi wanafahamu mantiki ya Uchaguzi wa amani.

Wakati akiyasema hayo, nae Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuwapatia eneo ili waweze kujenga Afisi ya Wilaya ya Kaskazini A kwani ni lengo la Tume kuwa na Afisi zenye hadhi ili ziweze kutoa huduma  kwa wananchi na ujenzi wake unapaswa kuanza mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Mhe.Ayoub Mohammed ameiahidi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwapatia eneo hilo karibu na Mkwajuni ili ujenzi wa Afisi hiyo uanze mapema kama utakavyotarajia.

Nae Mhe.Ayoub Bakar Hamad ambae ni miongoni mwa wajumbe wapya wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) alipata nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya Tume hiyo ambapo ameishukuru Afisi ya Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Unguja na Serikali kwa ujumla wake, kwani ndio mdau muhimu kwa Tume hiyo kwaiyo ni vyema kuendeleza mashirikiano kwa lengo la Tume ni kuifanya Nchi iwe na amani na iwe bora zaidi baaada ya Uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na mkutano huo, aliendelea na ziara yake  ambapo alikagua Afisi ya Magharibi A na B pamoja na  Kaskazini A na B za Tume hiyo.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii