Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imewataka Masheha na Mawakala wa Vyama vya Siasa kutoa elimu ya zoezi la Uandikishaji kwa wananchi ili kuepusha dhana hasi kwa utoaji wa huduma hiyo hasa pale vitambulisho vinaposhindwa kusoma katika mfumo.

Aliyasema hayo Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe.Ayoub Bakar Hamad wakati akizungumza na Masheha na Mawakala wa Vyama vya Siasa katika kituo cha Uandikishaji cha Skuli ya Utaani wakati wa zoezi la siku tatu la kukagua vituo vya Uandikishaji kwa Wilaya ya Wete.

Alisema zoezi la Uandikishaji Wapiga Wapya linakumbana na changamoto  kadhaa hasa changamoto  za kimfumo kwani Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inategemea taarifa za wananchi kutoka katika afisi ya ZAN ID na Tume iliingiza taarifa za wananchi mapema kabla ya zoezi kuanza hivyo wale ambao wameingizwa taarifa zao kwa siku za karibuni kuna uwezekano wa taarifa zao kutosoma katika mfumo kutokana na kukosekana kwa taarifa zao.

Alisema Mawakala wa Vyama vya Siasa na Masheha wamepewa mafunzo ya kuandikishwa ikiwa mtu amekataliwa kuandikishwa atatakiwa apewe fomu ya kukataliwa kuandikishwa hivyo ni vyema pia elimu hiyo kuwapatia wananchi ili kuwa na uelewa wa zoezi hilo.

Alisema Tume inatembelea maeneo mbalimbali ili kujua changamoto hizo hivyo ni vyema Mawakala Masheha waendelee kuelimishana ili wao wasiwe na dhana hasi pamoja na wananchi juu ya zoezi hili ambalo linafuata utaratibu wa kisheria na ikitokea Sheha amemkatalia mwananchi kumuandikisha na kama hana sifa  za ukaazi basi anapaswa kuwaeleza Mawakala kwa namna nzuri ili zoezi hilo liendelee kwa amani na utulivu.

Alisema Tume haiwezi kutumia gharama kubwa na kuzunguka katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kutowaandikisha wananchi bali wao wanataka kuona watu wanaandikwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ila wanataka kuona utaratibu unafuatwa na wao wataendelea kuzipokea changamoto hizo,

kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Utaani Sikitiko Hassan Ali aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kutembelea kituoni hapo na kusisitiza kuwa zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya kwa Shehia yake linaendelea vizuri na hakuna changamoto yeyote iliyojitokeza.

Nae Mkuu wa kituo cha Uandikishaji Suleiman Juma Suleiman alizungumzia baaadhi ya changamoto zinazolikabili zoezi hilo ikiwemo changamoto ya kimfumo ila changamoto hiyo imekuwa ikitatuliwa na wataalamu wa mifumo na zoezi hilo bado linaendelea vizuri na kuna mashirikiano mazuri kituoni hapo.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inaendelea na zoezi la kukagua vituo vya Uandikishaji kwa shehia mbalimbali za Unguja na Pemba ili kujua maendeleo ya zoezi hilo.

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii