Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mhe.Jaji Aziza Iddi Suwedi amefungua rasmi zoezi la Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya kwa awamu ya kwanza ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao wa 2025 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata haki ya kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi ujao.

Jaji Aziza ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea na kukagua zoezi la Uandikishaji la Wapiga Kura Wapya katika kituo kilichopo Msuka Mashariki  katika Wilaya ya Micheweni na kujionea namna zoezi hilo linavyofanyika.

 

“Zoezi kwa vituo tulivyovitembelea mpaka sasa  muitikio ni mzuri,watu wamejitokeza waliokuwa hawajaandikishwa na kila aliyefika kituoni na kuwa na sifa za kuandikishwa ameandikishwa na hadi muda huu hakuna tatizo lolote lililoripotiwana hakuna malalamiko tuliyoyapokea,tumezungumza na mawakala wote wa Vyama vya Siasa kwa vituo tulivyovitembelea wameshukuru na kwa pamoja wamesema zoezi linaendelea vizuri,niwaombe wale ambao hawajaandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura na wanavitambulisho vya Mzanzibar wajitokeze kuja kujiandikisha ili wapate haki yao ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa 2025” Alisema

Akizungumzia changamoto za zoezi hilo Mhe.Jaji Aziza Alisema hakuna changamoto kubwa iliyojitokeza katika zoezi hilo na changamoto chache zilizojitokeza hasa zinazohusu uingizaji wa alama za vidole (biometric) zimetatuliwa na timu  ya wataalamu wa mifumo (IT Supporters) ambao wapo vituoni humo.

Akizungumza juu ya zoezi hilo kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Thabit Idarous Faina  amewataka Wananchi kutosubiri siku ya mwisho ya zoezi la Uandikishaji katika Wilaya zao kuja kujiandikisha na ni busara kuwahi mapema kwani kusubiri siku ya mwisho kuna changamoto mbalimbali hivyo amewaomba wananchi kushiriki zoezi hilo mapema ili kupata fursa ya kushiriki Uchaguzi wa 2025.

Na kwa Upande wao Mawakala wa Vyama mbalimbali vya siasa wameishukuru Time ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa utaratibu mzuri uliowekwa kwa zoezi hilo na kuwataka wananchi kujitokeza kuja kujiandikisha.

 

Zoezi la Uandikishaji Wapiga Kura Wapya limeanza tarehe 2 Disemba 2023 katika Wilaya ya Micheweni ambapo Jumla ya vituo 25 katika Wilaya hiyo vimefunguliwa katika Shehia mbalimbali.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii