TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) inawaomba wananchi, wapiga kura wa Jimbo la Mtambwe, vyama vya siasa, wenye nia ya kugombea, na wadau wengine wa uchaguzi kujitayarisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba 28 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji George Joseph Kazi aliyasema hayo, alipokua akifungua Mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mtambwe, huko ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete Pemba, kufuatia kifo cha aliekua Mwakilishi wa Jimbo hilo Habibu Ali Mohamed kilichotokea Machi 3 mwaka huu.

Alisema kuwa, Tume ya uchaguzi chini ya kifungu cha 40 (2) (3) cha sheria ya uchaguzi namba Nne ya mwaka 2018 inajukumu la kuendesha uchaguzi mdogo kwa nafasi hiyo si chini ya miezi minne na si zaidi ya miezi 12.

"Mnamo Machi 6 mwaka huu tulipokea taarifa kutoka kwa Muheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi kuwepo wazi nafasi ya mjumbe wa Baraza hilo Jimbo la Mtambwe kilichotokea Machi 3 mwaka huu", alisema.

Aidha alisema, huo ni utaratibu wa Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kukutana na wadau wake kila linapotokea jambo muhimu la kitaifa linalohitaji ushirikishwaji wa wadau. 

Akitoa maelezo ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo Mkurugenzi wa uchaguzi Thabit Idarous Faina alisema,Tume kupitia msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo inatarajia kukamilisha baadhi ya taratibu za ununuzi wa vifaa vya kupigia kura, uchapishaji wa fomu na elimu ya wapiga kura

Hata hivyo, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuhakikisha wanakwenda katika vituo vya kupiga kura wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura na kwa ambao wamepoteza vitambulisho vyao wafike katika ofisi za Wilaya na kujaza fomu na kupatiwa kitambulisho hicho ndani ya siku tatu kabla ya uchaguzi.

Akitoa maelezo ya sheria katika uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo Mkuu wa Kurugenzi ya huduma ya sheria Maulid Ame Mohamed, mambo yanayokatazwa na sheria katika uchaguzi ni kujiandikisha zaidi ya mara moja, kutoa taarifa za uongo ili ateuliwe kuwa mgombea na kupiga kampeni za kibaguzi zinazohatarisha amani na usalama wa nchi.

"Naomba wananchi wa jimbo la Mtambwe kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya tume ya uchaguzi na kuendelea kuvibakisha Visiwa vyetu katika hali ya amani na utulivu", alisema.

 Wakichangia mada miongoni mwa wadau wa Mkutano huo Hidaya Mjaka Ali kutoka Jumuiya ya wanawake wenye ulemavu (JUWAUZA) ameiomba (ZEC) kuangalia miondombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu pamoja na kuwaekea wakalimani watakaowasaidia katika zoezi hilo.

 

Nae Asha Mohamed Ali kutoka chama cha UDP Mkoa wa Kusini Pemba alisema, wanawake wamekua wakishiriki kugombania nafasi mbali mbali za uongozi lakini wamekua wakikata tamaa na kurejeshwa nyuma kwa kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake Khamis Juma Abdalla kutoka chama cha wananchi (CUF) ameiomba (ZEC) kuandaa utaratibu mzuri katika uchaguzi huo bila ya ubaguzi ili kuondosha migogoro baina ya vyama pinzani vya Siasa baada ya kumalizika uchaguzi huo.

 

Uchaguzi mdogo wa jimbo la Mtambwe wadi ya Welezo Oktoba 1 hadi 7 kutakua na zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi, Oktoba 8 itakua siku ya uteuzi, 11 hadi 26 kutakua na kampeni za uchaguzi, Oktoba 28 kutakua na upigaji kura na utangazaji wa matokeo.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii