Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inatarajia kufanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani kwa Wadi ya Welezo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

 Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Mhe.Jaji George Joseph Kazi, alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano kwa wadau wa Uchaguzi, uliofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni,Mjini Unguja.

Alisema Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Wadi hiyo Ramadhan Ali Juma aliyefariki June 5 mwaka huu.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi namba nne ya mwaka 2018 Tume ya Uchaguzi inawajibika kufanya Uchaguzi ili kujaza nafasi hiyo iliyo wazi si chini ya miezi minne.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba Wananchi,Wapiga kura wa wadi, Vyama vya Siasa pamoja na wenye nia ya kugombea nafasi hiyo kujitayarisha na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi huo ili kupatikana kiongozi atakaeweza kushiriki katika harakati mbalimbali za kimaendeleo.

  

Akiwasilisha mada juu ya matayarisho ya Uchaguzi huo Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Ndugu.Thabit Idarous Faina alisema matayarisho ya uchaguzi huo yamekamilika na kusisitiza hakuta andikishwa Wapiga Kura wapya na badala yake watatumia orodha ileile iliyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 ya Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwaomba Wananchi siku ya Uchaguzi kufika katika Vituo wakiwa na vitambulisho vyao vya Kupigia Kura.

Alifahamisha kuwa Tume inaendelea kutoa elimu na kuwawezesha Wapiga Kura kujua Vituo vyao vya kupiga kura kwa kutumia simu ya Mkononi ili kuondosha sintofahamu wakati utakapofika.

Washiriki wa mkutano huo waliviomba Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutumia busara kipindi chote cha Uchaguzi ili kutoa nafasi kwa Vyama vya Siasa na Wananchi kutekeleza haki yao kwa ufanisi.

Mbali na hayo walivisisitiza Vyama vya Siasa kuacha mihemko ya siasa na badala yake kudumisha amani na utulivu ili nchi iendelee kuwa katika hali ya amani na utulivu.

 

Jumla ya mada mbili zimetolewa katika Mkutano huo ikiwemo matayarisho ya Uchaguzi huo Mdogo wa Wadi ya Welezo pamoja na nafasi ya Sheria katika Uchaguzi.

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii