Waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla wameaswa kuacha kabisa taarifa zinazotolewa katika mitandao ya kijamii ambazo zina nia ya kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini na badala yake wafuate vyanzo sahihi vya habari wakiwemo viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Hayo yalielezwa na Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Halima M. Said huko katika ukumbi Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi Pemba wakati akifunga Mkutano wa Wadau wa Uchaguzi kwa Makundi yenye Mahitaji Maalum juu ya Uendelezaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uandikishaji wa 2023 , waandishi wa habari wanapaswa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao na kufanya juhudi za makusudi za kuendelea kuiweka jamii ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika hali ya amani.

“ Kuna mambo mengi munaweza kuyasikia na kuyaona kwenye mitandao ya kijamii yanayohusiana na zoezi hili, tafadhalini musiyachukuwe na kuyatangaza bila ya kupata maelezo ya kina kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar “, alieleza.

Aliwaomba waandishi wa habari kuisaidia Tume hiyo kwa kufanya mijadala na vipindi maalumu juu ya Uandikishaji huo ili wananchi waweze kufahamu zaidi na kuwaelewa wanaohusika na zoezi hilo ili kuepuka misongamano kwenye vituo hivyo.

Mjumbe huyo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) aliwataka waandishi wa habari na wadau wengine kuendelea kudumiasha amani na utulivu ili iweze kudumu ndani ya nchi.

Kwa upande wa washiriki wa Mkutano huo waliipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha katika harakati za uendelezaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hiyo ni kuonesha ni kwa namna gani Tume imejipanga ili kuona kila mmoja anapata haki hiyo ya kidemokrasia.

Hata hivyo waandishi wa habari waliahidi kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa dhamira kubwa ya kulifanya zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa nchi kuona limefanikiwa kama ilivyotarajiwa.

   

 

 

Mawasiliano Yetu


Tume ya Uchaguzi Zanzibar

S.L.P 1001 - Zanzibar, Tanzania.

Simu: +255 242231489

Nukushi: +255 242233828

Mitandao ya Kijamii